1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama awawekea vikwazo viongozi wa Burundi

24 Novemba 2015

Rais Barack Obama wa Marekani amewawekea vikwazo viongozi wanne wa Burundi akiwemo waziri wa usalama Alain-Guillaume Bunyoni kwa kubeba jukumu la machafuko yanayoikumba nchi hiyo tangu Aprili mwaka huu.

https://p.dw.com/p/1HB7b
Matumizi ya nguvu yanapamba moto nchini BurundiPicha: Reuters/G. Tomasevic

Vikwazo hivyo vinawahusu viongozi wawili wa serikali mjini Bujumbura pamoja pia na madhamana wawili wa njama ya mapinduzi ya kijeshi yaliyoshindwa mwezi may mwaka huu.

Tangazo hilo limetolewa wakati waziri wa mambo ya ndani wa Burundi ametangaza kusitishia kwa muda shughuli za mashirika kumi ya kiraia.Mashirika hayo yalikuwa mstari wa mbele miongoni mwa wale waliokuwa wakipinga mhula wa tatu wa rais Nkurunziza.Yanaandamwa na viongozi wa serikali kwa madai ya "uasi" na wengi wa viongozi wa mashirika hayo wamekimbilia uhamishoni.

Vikwazo vya rais Obama-vinavyowapiga marufku viongozi hao wa Burundi kuingia nchini Marekani na mali zao kuziwiliwa-vimefuatia vile vilivyotangazwa mapema mwezi uliopita wa October na Umoja wa ulaya.

"Haviwahusu wananchi wa kawaida wa Burundi",bali baadhi ya watu serikalini wanaochangia kupalilia ghasia,kudhoofisha taasisi za kidemokrasi na kujibebesha jukumu la visa vinavyokwenda kinyume na haki za binaadam" taarifa ya ikulu ya Marekani imesema.

Marufuku yanamhusu pia mkuu wa zamani wa vikosi vya wanajeshi

Miongoni mwa waliotajwa kuwekewa vikwazo hivyo ni pamoja na naibu mkurugenzi wa polisi ya taifa Godefroid Bizimana ambae pia ametajwa katika orodha ya watu waliowekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya.Kwa mujibu wa serikali mjini Washington,Godefroid Bizimana ndie aliyeongoza opereshini za polisi kukandamiza maandamano ya amani ya upande wa upinzani na kutumia nguvu kupita kiasi.

Flüchtlingscamp Nyarugusu Tansania
Mikururo ya wakimbizi wa Burundi katika kambi ya Nyarugusu TanzaniaPicha: DW/P. Kwigize

Mwengine ni Godefroid Niyombare,aliyekuwa kiongozi wa idara ya upelelezi na pia kiongozi wa zamani wa vikosi vya jeshi,pamoja na waziri wa zamani wa ulinzi Cyrille Ndayirukire.

Jenerali Niyombare ndie aliyeongoza njama ya mapinduizi yaliyoshindwa mwezi may uliopita na tangu wakati huo amekimbia akiahidi kumpindua rais Nkurunziza.

"Burundi inakurubia kutumbukia katika janga la maafa,lakini kuna njia moja ambayo viongozi wanaweza kuitumia kupata ufumbuzi wa kisiasa"amesema msemaji wa baraza la usalama wa taifa nchini Marekani Ned Price.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa akosoa uamuzi wa kupigwa marufuku mashirika ya kiraia

Mjini Bujumbura kwenyewe,shughuli za mashirika muhimu ya kiraia zimepigwa marufuku."Hatua hii inamaanisha moja kwa moja kwamba mashirika yasiyomilikiwa na serikali yamepigwa marufuku kuendesha shughuli zao-hadi mahakama itakapoamua" afisa mmoja wa wizara ya mambo ya ndani ambae hakutaka jina lake litajwe.Mashirika hayo kumi yaliyopigwa marufuku yanalenga shughuli zake katika kupigania haki za binaadamu,kupambana na rushwa na kuwapatia misaada kwa watoto.

Burundi Pierre-Claver Mbonimpa Menschenrechtsaktivist
Mwanaharakati wa haki za binaadam Pierre-Claver MbonimpaPicha: Getty Images/AFP/A. Vinceno

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki Moon amelaani uamuzi huo.Mshauri maalum wa katibu mkuu nchini Burundi amewasili jana mjini Bujumbura na amepangiwa kuzungumza na viongozi wa nchi hiyo kabla ya kuwasilisha ripoti yake kuambatana na azimio la baraza la usalama kuhusu Burundi lililopitishwa novemba 12 iliyopita.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AP/Reuters

Mhariri:Yusuf Saumu