1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama na mahkama za Guantanamo

15 Mei 2009

Tume za mahkama ya kijeshi kuendelea ?

https://p.dw.com/p/Hr06
Wafungwa GuantanamoPicha: AP / DW

Utawala wa Rais Barack Obama nchini Marekani, utatangaza leo kuendeleza zile Tume za kijeshi za enzi ya utawala wa Bush zinazowahukumu watuhumiwa wa ugaidi. Hata hivyo, sheria za kuwakinga zitakuwa bora. Hatua hii iliokwishazusha upinzani kutoka wakereketwa wanaotetea haki, inabainisha jinsi utawala wa Obama unavyotatanika kati ya hoja za usalama wa taifa na za kisheria katika vita vya kupambana na ugaidi ulimwenguni. Ramadhan Ali na ripoti zaidi.

Rais Obama alisimamisha mahkama za kijeshi za Gereza la Guantanamo mara tu baada ya kushika madaraka akipanga kuzikagua upya zinavyofanya kazi. Obama alidai wakati ule kwamba mfumo uliotumiwa haukufanya kazi barabara, lakini hakuondoa uwezekano wa kurekebisha mahkama hizo.

Afisa mmoja wa utawala wa Obama ambae hakutaka kutajwa, amesema tangazo juu ya mfumo mpya wa mahkama za kijeshi litatolewa leo. Mfumo mpya wa klisheria wa kuwashtaki wale watuhumiwa maarufu tu wa Al qaeda ambao wako gerezani Guantanamo,kisiwani Kuba,utajumuisha kutoruhusu ushahidi wa kusikia tu kutumiwa dhidi ya wafungwa. Mageuzi pia yataingiza kutoruhusu ushahidi uliopatikana kwa njia za mateso mfano wa mtindo wa kumfanya mtuhimiwa kana kwamba anazama majini pamoja na mbinu nyengine zinazotumiwa na shirika la ujasusi la marekani (CIA) kujipatia habari.

Hatua hizi zitawahusu wafungwa watano miongoni mwa wengine, wanaotuhimiwa kuandaa ile njama ya shambulio la Septemba 11,2001.Miongoni mwao - ni jogoo lao Khalid Sheikh Mohammed.

Warepublican wamekosoa mno amri ya Rais Obama ya kulifunga gereza la Guantanamo hapo Januari mwakani na wademocrats wamekataa ombi la Ikulu kutoa fedha za kugharimia mpango wa kulifunga kabisa.

Gereza la Guantanamo lililopata umashuhuri duniani kote likifungamana na vita vya rais George Bush vya kupambana na ugaidi,lingali lina wafungwa 241 kutoka nchi 30 mbali mbali .

Kwa wiki kadhaa, warepublican wamekuwa wakimhujumu rais Obama kwa amri yake ya kulifunga gereza hilo na kwa kusimamishwa mahkama za kijeshi.Wakidai kuwa rais Obama hakuwa na mipango nini afanye kwa wafungwa.

Seneta John McCain wa chama cha Republican, alieongoza utungaji wa sheria ya kuunda Tume hizo za mahkama ya kijeshi ,amesema Tume za mashtaka ndio njia pekee inayofaa kuwashtaki watuhumiwa na kwamba anashirikiana na Ikulu mjini Washington juu ya jinsi ya kuziendeleza mbele.

Afisa wa utawala wa Obama amesema rais akiungamkono mara kwa mara Tume hizo za kijeshi kama mojawapo ya njia za kuwahukumu wafungwa,lakini akiamini mtindo uliotumiwa na utawala wa Bush haukutoa ulinzi wa kutosha kwa wafungwa.Mfumo uliotumika uliwahukumu watuhumiwa 3 tu katika kipindi cha miaka 8.

Baadhi ya vikundi vya wakereketwa wa haki za binadamu , vimedai kuwa utawala wa Obama, uwashtaki watuhumiwa chini ya mfumo wa kawaida wa sheria za Marekani.Wapinzani wake wameonya kuwa, ushahidi uliopatikana kwa njia za mabavu,hautasimama mbele ya mahkama kama hizo.

Muandishi: Ramadhan Ali /AFPE

Mhariri: J.Charo