1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama na Putin kukutana licha ya mvutano

Admin.WagnerD11 Novemba 2014

Rais Obama wa Marekani na Putin wa Urusi walikutana Jumanne mjini Beijing, kandoni mwa mkutano wa Jumuiya ya Ushirikisho wa Kiuchumi ya nchi za Asia na Pasifik - APEC . Kuzungumzia masuala ya Iran ,Syria na Ukraine.

https://p.dw.com/p/1DlNV
Rais wa Marekani Barack Obama na wa Urusi Vladimir Putin.
Rais wa Marekani Barack Obama na wa Urusi Vladimir Putin.Picha: Reuters

Uhusiano baina ya Marekani na Urusi uko katika kiwango cha chini kabisa tangu kumalizika enzi ya vita baridi, huku Urusi ikiekewa vikwazo vinavyoongozwa na Marekani kutokana na hatua yake ya kulitwaa eneo la Ukraine la Crimea mwaka huu, pamoja na mchango wake katika vita vya wale wanaotaka kujitenga mashariki mwa Ukraine.

Marais hao wawili hata hivyo walikutana kwa mazungumzo yasio rasmi kwa karibu dakika 15 hadi 20 wakati wa mkutano huo wa kilele wa APEC kaskazini mwa mji mkuu wa China.

Nchi zote mbili-Marekani na Urusi- zinahusika katika mazungumzo kati ya madola matano yenye nguvu pamoja na Ujerumani kwa upande mmoja na Iran upande wa pili , kuhusiana na mpango wa nyuklia wa Iran. Lakini kuhusiana na Syria Urusi ni mshirika wa karibu wa utawala wa Rais Bashar al-Assad, na imemuunga mkono katika kipindi chote cha vuguvugu lililoanza Machi 2011 dhidi ya utawala wake.

Tafauti baina ya Marekani na Urusi juu ya Ukraine

Lakini tafauti kubwa za mtazamo hivi sasa kati ya Marekani na Urusi ni kuhusiana na Ukraine. Katikati ya mwezi Oktoba Putin alimshutumu Obama kuwa anajenga tabia ya uhasama dhidi ya Urusi, wakati Obama alikosoa kile alichokiita "uchokozi," wa Urusi dhidi ya Ulaya wakati alipolihutubia Baraza kuu la Umoja wa Mataifa.

APEC Gipfel Putin und Obama 11.11.2014 Peking
Rais wa Marekani Barack Obama na wa Urusi Vladimir Putin.Picha: Reuters//Press service of the president of the Russian Federation/RIA Novosti

Hapo mapema naibu waziri wa Marekani anayehusika na usalama wa taifa Ben Rhodes, aliwaambia waandishi habari mjini Beijing kwamba " tunaendelea kusumbuliwa na harakati za Urusi katika Ukraine na ikiwa zitaendelea ni sababu moja ya kuitenga."

Wakati mkutano wa kilele wa APEC mjini Beijing, umemalizika Obama na Putin pia watahudhuria mkutano wa kilele mataifa 20 yenye nguvu kiuchumi, kundi linalojulikana kama G20. Mkutano huo utafanyika mjini Brisbane-Australia tarehe 15 na 16 Novemba. Hata hivyo haikufahamika ikiwa huko nako watakutana tena kwa mazungumzo mengine kandoni mwa mkutano huo.

Ikulu ya Marekani imeshasema kwamba sawa na ilivyokuwa mjini Beijing , hakuna mpango wowote wa Obama kukutana na Putin kwa mazungumzo rasmi.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, AFP

Mhariri:Hamidou Oummilkheir