1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Obama, Netanyahu waendelea kutafautiana juu ya Iran, Mashariki ya Kati

4 Machi 2014

Rais Barack Obama amemuhakikishia Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kwamba bado Marekani imedhamiria kuizuia Iran kuwa na silaha za nyuklia lakini akimtaka naye kudhamiria kweli amani na Wapalestina.

https://p.dw.com/p/1BJBM
Netanjahu Obama Israel USA 03.03.2014
Rais Barack Obama wa Marekani (kulia) akizungumza na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, mjini Washington Jumatatu ya tarehe 3 Machi 2014.Picha: picture-alliance/AP

Obama na Netanyahu, ambao wamekuwa na uhusiano wa mashaka katika siku za hivi karibuni, walijitahidi kutoonyesha wazi mvutano uliopo baina yao, wakati walipokaa pamoja kuzungumza na waandishi wa habari.

Hata hivyo, mwandishi wa shirika la habari la Reuters amesema tafauti kati yao zilikuwa wazi, na hata baada ya mazungumzo kumalizika masaa matatu baadaye, hakukuwa na ishara yoyote ya maendeleo.

Katika mkutano huo walioufanya kabla ya mazungumzo yao rasmi kuanza hapo jana (03.02.2014), Netanyahu alimueleza wazi Obama kwamba kamwe hatouweka rehani usalama wa Israel, licha ya rais huyo wa Marekani kumjengea imani kwa diplomasia inayotumika kwenye majadiliano ya mpango wa nyuklia wa Iran.

"Changamoto kubwa hapana shaka ni kuizuia Iran kuwa na uwezo wa kutengeneza silaha za nyuklia. Nadhani lengo hilo linaweza kufikiwa kwa kuizuia Iran kurutubisha madini ya urani na kuvunja vinu vyake vyote vya nyuklia. Sijui ikiwa lengo hilo linaweza kufikiwa kwa amani na kupitia diplomasia, lakini naweza kukwambia kwamba hakuna nchi iliyo hatarini zaidi kuliko Israel." Alisema Netanyahu.

Suala la Mashariki ya Kati

Netanyahu aliwasili mjini Washington kukiwa tayari na onyo la Obama kwamba itakuwa vigumu zaidi kuilinda Israel dhidi ya hatua za kuitenga kimataifa, ikiwa juhudi za amani za Mashariki ya Kati zitashindwa.

Rais Barack Obama wa Marekani (katikati) akiwakutanisha Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu (kushoto) na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina mjini New York mwezi Septemba 2009.
Rais Barack Obama wa Marekani (katikati) akiwakutanisha Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu (kushoto) na Rais Mahmoud Abbas wa Palestina mjini New York mwezi Septemba 2009.Picha: picture-alliance/AP

"Ninaamini kwamba inawezekana kabisa kuunda madola mawili huru, dola ya Kiyahudi ya Israel na dola ya Palestina, ambamo watu wataishi kwa ujirani na amani na usalama. Lakini hilo ni jambo gumu na linalohitaji kujitolea kwa pande zote mbili." Rais Obama alirejelea msisitizo huo kwenye mkutano huo na waandishi wa habari.

Obama alionya kwamba hakuna muda mrefu sana uliobakia na hivyo kumtaka Netanyahu kufanya "uamuzi mgumu" kusaidia kuyaokoa mazungumzo ambayo hadi sasa yanaonekana kushindwa.

Wakati mazungumzo hayo ya amani yalipoanza tena mwezi Julai mwaka jana, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, aliweka muda wa mwisho kwa pande zote mbili kufikia makubaliano kuwa ni mwishoni mwa mwezi Aprili mwaka huu, lakini uamuzi wa Israel kuendelea na mradi wake wenye utata wa kujenga makaazi ya walowezi kwenye ardhi za Wapalestina umeyakwamisha.

Kerry amekwisha kiri kwamba hakuna matumaini ya kufikiwa kwa makubaliano na sasa anapigania kupatikana angalau kwa mpango wa utaratibu wa mazungumzo kati ya pande hizo mbili.

Baadaye Netanyahu alikuwa na mazungumzo na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Marekani na hivi leo anatazamiwa kuzungumza kwenye mkutano wa kundi maarufu la waungaji mkono wa Israel nchini Marekani, AIPAC.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP
Mhariri: Daniel Gakuba