1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ocampo awataja wafadhili 6 wa ghasia za uchaguzi Kenya

15 Desemba 2010

Louis Moreno Ocampo amewataja watu hao sita, katika mkutano wa waandishi wa habari mjini The Hague saa sita mchana

https://p.dw.com/p/QYmo
Mwendesha mashtaka mkuu wa ICC, Luis Moreno OcampoPicha: AP

Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Uhalifu, ICC ilio na makao yake mjini The Hague Uholanzi leo mchana (15.12.2010) amewataja watu sita, washukiwa wakuu wanaodaiwa walihusika na kufadhili machafuko ya baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 nchini Kenya.

Ocampo amewawasilishia rasmi kwa majaji wa mahakama hiyo majina ya watuhumiwa hao waliopanga njama iliyosababisha ghasia baada ya uchaguzi mkuu. Miongoni mwa waliotajwa ni Naibu Waziri Mkuu Uhuru Kenyatta na Waziri wa zamani wa Elimu ya ngazi za juu William Ruto. Tukio hilo limezua mitazamo tofauti ndani ya Kenya.

Luis Moreno Ocampo baadaye ameitaka mahakama hiyo iwatolee watuhumiwa hao wito wa kufika mahakamani. Ocampo pia ametoa masharti kadhaa ikiwemo, baada ya kutajwa majina yao, watu hao sita watatakiwa kuwasiliana mara kwa mara na mahakama hiyo ya ICC.

Bwana Ocampo alisema iwapo washukiwa hao watakiuka masharti hayo, basi ataitaka mahakama hiyo ya ICC kutoa waranti wa kuwakamata. Mwezi Machi mwaka huu, Mahakama hiyo ya uhalifu ya ICC iliidhinisha uchunguzi uanzishwe kuhusiana na ghasia hizo za uchaguzi nchini Kenya baada ya kiongozi wa upinzani wakati huo Raila Odinga kudai kuwa Rais Mwai Kibaki alifanya hila katika uchaguzi huo uliomrejesha tena madarakani.