1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ODM chashinda mbio za kumtafuta Spika wa Bunge la Kenya

16 Januari 2008
https://p.dw.com/p/CqDC

NAIROBI:

Bunge la Kenya limemchagua mbunge wa upinzani kama Spika wa bunge hilo.

Hiki ndicho kikao cha kwanza cha bunge hilo kufanyika tangu kuchaguliwa tena kwa rais Mwai Kibaki katika uchaguzi ambao ulizusha utata.Spika mpya ni Kenneth Marende,wakili mwenye umri wa miaka 52.Kabla ya kupiga kura kumchagua spika mpya-kulitokea majibizano ya maneno makali kati ya wabunge wa upande wa serikali na wale wa upinzani unaongozwa na Raila Odinga.Uchaguzi wa Spika ulikuwa wa vuta nikuvute.Ililazimika kufanyika kwa awamu tatu kuweza kupata mshindi.Pambano lilikuwa kati ya mjumbe wa chama cha ODM Kennedy Marende na mjumbe anaeungwa mkono na chama tawala cha PNU Francis Ole Kaparo ambae alikuwa anatafuta muhula wa nane kama Spika nafasi alioshikilia kwa kipindi cha miaka 15.Tangazo la ushindi lililotangazwa na karani wa bunge Samuel Ndindiri lilipokelewa kwa shangwe na upande wa upinzani .

Katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa-Kofi Annan alikuwa aende Kenya kujaribu kupatanisha serikali na upinzani,lakini safari yake hii imeahirishwa kwa siku kadhaa.Serikali ya Kenya imekataa upatanishi wa Bw Annan. Umoja wa Ulaya umeonya kuwa utazuia msaada wake kwa Kenya ikiwa juhudi za upatanishi zitashindwa.

Kwa wakati huohuo chama cha upinzani cha ODM kinapanga kufanya mikutano kadhaa nchini Kenya kwa siku tatu mfululizo kuanzia hii leo kama ishara ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa mwezi jana ambao ulimpa rais Kibaki muhula wa pili.Hata hivyo serikali imepiga marufuku mikutano yote nchini humo kufuatia ghasia za kisiasa na kikabila zilizofuatia uchaguzi ambapo watu wanaofikia 600 walipoteza maisha yao.