1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uwindaji haramu Afrika wapelekea ndovu kubadili tabia zao

22 Septemba 2017

Kutokana na ongezeko la uwindaji haramu barani Afrika, ndovu katika maeneo hayo wamebadili mwenendo wa tabia yao ya kuonekana mchana na badala yake wanajificha wakati huo na kujitokeza usiku ili kuepuka wawindaji haramu.

https://p.dw.com/p/2kXt7
Galerie - Der Klimawandel und seine Folgen
Picha: picture-alliance/AP Photo

Visa vingi vya uwindaji haramu Barani Afrika vimepelekea ndovu wa Afrika mashariki kuvumbua njia ya kujiokoa dhidi ya wawindaji haramu, kulingana na utafiti mpya.

Kulingana na watafiti, ndovu hao wamebadili tabia yao ya kutembea mchana na badala yake wanajificha wakati huo na kujitokeza usiku ili kujinusuru.

Kwa kawaida ndovu hutafuta chakula na kutembea wakati wa mchana huku wakipumzika chini ya kivuli.

Lakini imeonekana kuwa ongezeko la visa vya uwindaji haramu inayotokana na biashara ya pembe za ndovu duniani, kumewapelekea wanyama hao kubadilisha tabia zao za toka jadi.

Kwa mujibu wa mtafiti kutoka chuo kikuu cha Twente nchini Uholanzi bwana Festus Ihwagi,  uwindaji haramu ukitekelezwa mchana, mabadiliko hayo ya tabia yanaonekana kuwa matokeo ya moja kwa moja ya viwango vya uwindaji haramu vinavyoendelea.

Katika utafiti huu, matokeo haya ya bwana Ihwagi yametokana na data  uilizokusanwa kutoka ndovu 60 kaskazini mwa Kenya waliofuatiliwa kupitia vifaa vya GPS kwa muda wa miaka mitatu wakati wa mwaka 2002 hadi 2012.

Akifanya kazi na shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na kuokoa ndovu ambalo limewavisha zaidi ya ndovu 100 vifaa vya GPS, Bwana Ihwagi alifuatilia harakati za ndovu wa kike 28 na wakiume 32 ndani na karibu ya maeneo ya Laikipia na Samburu .

Ikabainika kuwa ndovu wa kike wanaishi kwa ukaribu na familia zao na mara nyingi watoto wakiwa karibu yao huku wanaume wakijitenga na kutembea kivyao.

Ili kutoa taswira mwafaka ya kufikia utafiti huu,  Ihwagi alilinganisha data mbili iliopima umbali ndovu hao wanatembea mchana na usiku na ya pili kutoka mabadiliko yaliotokea kuhusu mauaji ya ndovu kutokana na uwindaji haramu.

Elefanten im in Krüger National Park
Ndovu wakikata kiu yao mtoniPicha: Getty Images

Imebainika kuwa matembezi ya usiku ya ndovu yaliongezeka sambamba na viwango vya uwindaji haramu haswa kwa ndovu wa kike.

Katika maeneo yalio hatari, ndovu wa kike wanapunguza shughuli zao za mchana kwa asilimia 50 ikilinganishwa na maeneo ambayo sio hatari. Kubadilisha tabia yao kwa njia hii kunaweza kusaidia kuwaweka ndovu hai kwa muda mfupi ujao lakini inaweza kuathiri pakubwa maisha yao, amesema mtafiti huyo.

Licha ya uwerevu wao, mfumo wao  wa kuzaliana unaweza kupunguza uwezo wao wa  kukabiliana na hali hii.

Kwa akina mama waliyo na watoto wadogo, hatari ya kushambuliwa na simba au fisi ni kubwa  wakati wa usiku, amesema  Ihwagi.

Kwa ndovu wakongwe, inaonyesha mabadilko ya maisha yao ya kawaida.

Vifaa vya GPS vinaweza kutumika kama mfumo wa kutoa onyo mapema ili kuwatahadharisha wanamazingira na wanaohifadhi mbuga za wanyama. Safari ya ghafla ya usiku kwa mfano kunaweza kuonyesha kwamba ndovu wanatishika.

Kulingana na muungano wa kimataifa kwajili ya kuhifadhi maumbile IUCN, idadi ya ndovu barani Afrika imeshuka kwa karibu 111,000 hadi 415,000 katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.

Mauaji ya ndovu haionyeshi dalili ya kupungua na karibu ndovu 30,000 wakiuliwa kwajili ya pembe zao kila mwaka, ili kukidhi mahitaji katika soko la bara Asia kwajili ya bidhaa zinazotokana na pembe na kutumiwa kama kwa ajili ya tiba za asili.

Kuongezeka kwa uwindaji haramu limekuwa tishio kubwa kwamaisha ya ndovu, anasema mtafiti  Ihwagi .

Matokeo haya yatachapishwa katika jarida la  uhifadhi wa mazingira mwezi Januari.

Mwandishi: Fathiya Omar

Mhariri:  Mohammed Abdul-Rahman