1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

OPEC Yaadhimisha mwaka wa 50 tangu kuasisiwa

Sekione Kitojo14 Septemba 2010

Shirika la mataifa yanayosafirisha kwa wingi mafuta, OPEC leo linaadhimisha miaka 50 tangu kuundwa kwake.

https://p.dw.com/p/PC4k

Shirika la mataifa yanayosafirisha kwa wingi mafuta , OPEC leo linaadhimisha miaka 50 tangu kuundwa kwake. katika kuadhimisha siku hii katibu mkuu wa Shirika hilo Abdulla el -Badri amesema OPEC haifurahishwi na kile inachoona kuwa ni ushindani usiokuwa wa haki kutoka kwa vyanzo vya nishati mbadala ambavyo vinapatiwa ruzuku.

Wataalamu wamegundua kuwa kuongezeka kwa nishati endelevu , ni moja ya changamoto ambazo nchi hizo 12 wanachama wa shirika la mataifa yanayosafirisha mafuta kwa wingi linakabiliana nayo katika miaka ijayo. Katibu mkuu wa OPEC Abdalla el-Badri alikuwa akizungumzia sera za serikali , hususan katika mataifa ya magharibi , kuongeza upatikanaji wa nishati mbadala, kutoza kodi mafuta yanayochimbwa ardhini na kutoa msaada kwa vyanzo vya nishati endelevu.

Hilo hatuliungi mkono, amesema katibu mkuu huyo, na kuongeza kuwa shirika lake linataka ushindani wenye masharti ambayo ni sawa katika soko lote la nishati.

Lakini el-Badri hana wasi wasi juu ya hali ya baadaye ya OPEC na mafuta. Mahitaji yanaongezeka, tusisahau hilo, amesema , akizungumzia hususan kwa mahitaji ya uchumi wa mataifa ya Asia.

Kwa upande mwingine katibu huyo wa shirika la OPEC amesema changamoto kubwa kwa shirika lake ni ulinzi wa mazingira, kubadilika kwa hali ya soko pamoja na vyanzo vipya vya fedha kwa wanachama wake.

Katika mahojiano katika gazeti la kila siku la Asharq al-Awsat, Abdalla el-Badri pia amesema kuwa kundi hilo lenye mataifa 12 wanachama halifikirii kuongeza wanachama wapya.

El-Badri amesema kuwa OPEC inaunga mkono juhudi za kubadilisha vyanzo vya nishati kuwa vya nishati mbadala kwa ajili ya mahitaji ya umeme na mengineyo na kudokeza kuwa dunia inahitaji kukubali ukweli kwamba mafuta yatakwisha siku moja. Lakini amesema mafuta yataendelea kuwa muhimu kwa miaka mingi ijayo.

Kutokana na matarajio ya kufanyika mikutano miwili ijayo ya mawaziri wa OPEC ambayo imepangwa kufanyika mwaka huu, katibu huyo mkuu hakuweza kutabiri iwapo uzalishaji utapunguzwa. Lakini amesema kuwa kwa sasa , shirika hilo halitaki kuvuruga mambo, katika ufufuaji wa uchumi duniani, awamu ambayo maafisa wa OPEC wametumia katika siku za nyuma kuashiria uzalishaji wa mafuta ambao haukubadilika. OPEC iliasisiwa mjini Baghdad hapo Septemba 14, 1960 na nchi za Iran, Iraq, Kuwait, Saudi Arabia na Venezuela, katika juhudi za kujitoa katika udhibiti wa mafuta yao kutoka kwa makampuni ya mataifa ya magharibi.

El-Badri amesema kuwa katika miaka 50 iliyopita , mataifa ya OPEC yameweza kudhibiti maliasili yao, yametoa mafunzo kwa wataalamu wao wa mafuta na mafundi, na wameunda makampuni yao ya kitaifa ambayo yanadhibiti uzalishaji.

Mwandishi : Sekione Kitojo / DPAE / APE

Mhariri : Mohammed Abdul Rahman