1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Operesheni ya Kupambana na Ugaidi.

Halima Nyanza/Reuters16 Aprili 2009

Wakati Juhudi za kupambana na Maharamia zikishika kasi, Marekani imesema itatuma mjumbe wake kushiriki katika Mkutano utakaofanyika wiki ijayo, ambao utaizungumzia Somalia kwa lengo la kupambana na tatizo hilo.

https://p.dw.com/p/HYDz
Wanajeshi wa Kupambana na Uharamia, wakiwasindikiza Maharamia wa Kisomali kujibu mashtaka yanayowakabili.Picha: picture-alliance/dpa

Akizungumza na Waandishi wa Habari mjini Washngton Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani Hillary Clinton amewaita Maharamia hao kuwa ni Wahalifu, kutokana na kwamba ni makundi ya watu wanaotumia silaha baharini kwa ajili ya kufanya uhalifu.


Amesema watu wote hao wanaopanga mashambulizi ni lazima wadhibitiwe na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.


Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani amesema kunahitajika makubaliano dhabiti kimataifa katika kupambana na Uharamia na ndio sababu anatuma mjumbe wao katika mkutano wa Wafadhili utakaoizungumzia Somalia ambao utafanyika Brussels Ubelgiji Ijumaa ijayo, Aprili 23.

wetu atashirikiana na washirika wetu kusaidia Wasomali kutusaidia kuzigundua kambi za maharamia na katika kupunguza na kuwapunguzia hamu vijana wa Kisomali kujiingiza katika Uharamia....''


Aidha Waziri wa Mambo ya nchi za Nje wa Marekani amesema nchi yake itaongeza juhudi za kuwasaka na kudhibiti masuala yote ya fedha ya maharamia hao, kama ilivyofanya wakati wa kupambana na wafanyabiashara haramu wa dawa za kulevya na makundi ya kigaidi.


Ameongezea kusema kwamba wamegundua kuwa maharamia wakuwa wakizidi kununua vifaa vya kisasa katika kufanyia uharamia huo.


Maharamia wanaotumia silaha nzito kutoka Somalia, nchi ambayo kwa sasa inakabiliwa na machafuko, wamekuwa wakiongeza kufanya mashambulio katika njia ya misafara ya Meli kwenye bahari ya hindi na katika njia muhimu ya misafara hiyo katika eneo la Ghuba ya Aden, wakikamata meli kadhaa na kuwakamata mateka mamia ya watu, huku wakidai mamilioni ya Dola kuwaachia.


Katika Operesheni hizo zinazofanywa Jeshi la Majini la Ufaransa pia kilifamikiwa kuwakamata Maharamia wa Kisomali waliokuwa wakijaribu kuteka meli iliyokuwa ikipeperusha bendera ya Liberia, baada ya helikopta ya jeshi la nchi hiyo kufanikiwa kuzuia shambulio hilo.


Manowari za kivita za Ufaransa zipo katika ukanda huo pia ikiwa ni sehemu ya Operesheni ya Atalanta ya Umoja wa Ulaya katika kupambana na uharamia, ambayo pia inayahusisha majeshi ya Ujerumani, Hispania, na Italia.


Katika hatua nyingine Balozi wa Misri nchini Somalia Said Morsi amesema nchi yake inawasiliana na viongozi wa kikabila na viongozi wengine wenye mamlaka nchini humo, kuweza kushinikiza kuachiwa kwa meli mbili za nchi hiyo zilizokamatwa wiki hii.


Licha ya Jeshi la Marekani kuwaua maharamia watatu wa Kisomali na kufanikiwa kumuokoa raia wa nchi yao aliyekuwa akishikiliwa na maharamia hao kwa muda wa siku tano, lakini bado matukio ya kutekwa nyara kwa meli na maharamia hao bado hayajapungua.

Mwandishi: Halima Nyanza

Mhariri: Aboubakar Liongo