1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Padiri wa Kanisa Katoliki apatikana na hatia kuhusika na mauaji ya 1994 nchini Rwanda

Mohammed Abdul-Rahman13 Desemba 2006

Ahukumiwa kifungo cha miaka 15 jela amepatikana na makosa ya kuwaamuru wanamgambo kulichoma moto Kanisa lililokua na watu 2,000 ndani waliokimbia kutafuta hifadhi.

https://p.dw.com/p/CHlv

Padiri huyo wa Kikatoliki Athanese Seromba, aliyehukumiwa kifungo cha miaka 15 jela, sasa atatumikia miaka 11 baada ya tayari kuwa gerezani kwa muda wa miaka minne. Kwa mujibu wa mashitaka yaliomkuta ana hatia, padiri huyo aliwaamuru wanamgambo wa Kihutu“Interahamwe“,waliokua na silaha za kienyeji kulishambulia kanisa na kuliwasha moto, huku polisi wakitupa mabomu ndani ya kanisa hilo mlimo kuwemo umati wa watu 2,000 waliokimbilia kujinusuru na mauaji. Baada ya kushindwa kuwauwa wote kanisani, Seromba akaamrisha kanisa livunjwe.

Kutokana na kisa hicho maelfu ya Wanyarwanda wameliacha mkono kanisa Katoliki, wakikasirishwa na kuhuzunishwa na madai ya kuhusika kwa baadhi ya maafisa wa kanisa hilo katika mauaji ya halaiki yaliodumu siku 100, ambapo zaidi ya watutsi 500,000 waliuwawa na wahutu wa msimamo mkali. Mapadiri , watawa na wafuasi wao walihusishwa na mauaji hayo, na baadhi ya makanisa yakageuka vituo vya mauaji.

Wakati kesi dhidi ya Seromba mwenye umri wa miaka 43 ilipokua ikiendelea, mawakili wake walilalamika kwamba anaandamwa kwa sababu tu ni mhubiri na kukumbusha kwamba baada ya vuta nikuvute ya muda mrefu kutaka apelekwe Arusha kwenye mahakama hiyo,Seromba alijisalimisha mwenyewe kwa mahakama hiyo ya kimataifa 2002, ili haki itendeke.

Kesi hiyo ilioanza Septemba 2004, ilikumbwa na uchelewesha na mabishano, ikiwa ni pamoja na jaribio lisilofanikiwa la upande wa utetezi mwezi Mei kutaka majaji watatu waliosikiliza kesi hiyo waondolewe, ukidai walikua na upendeleo.

Seromba ni padiri wa kwanza wa kikatoliki, kuhukumiwa na mahakama hiyo ya kimataifa ya Arusha kuhusu mauaji ya Rwanda, ingawa kesi ya padiri mwengine wa Kanisa la Andventist Emmanuel Rukundo, mhubiri wa zamani jeshini kaskazini mwa Rwanda imeanza tangu mwezi uliopita.

Kesi ya tatu inasubiriwa kuanza na tayari pia wahubiri wengine na watawa wameshahukumiwa nchini Rwanda na katika mahakama za nje.

Wiki iliopita,mhubiri Elizaphan Ntakirutimana aliyehukumiwa na mahakama ya kimataifa ya Arusha kifungo cha miaka 10 jela, alikua mkosa aliyehukumiwa na mahakama hiyo kuachiliwa huru, baada ya kumaliza kifungo chake.

Tangu ilipoundwa 1994, mahakama hiyo mjini Arusha-Tanzania, imeshawahukumu watu 31 kwa makosa ya kuandaa au kutekeleza mauaji. 26 kati yao walipatikana na hatia na watano wakaachiliwa huru.