1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pakistan yaapa kuwachukulia hatua wanamgambo wa Taleban

Jason Nyakundi24 Aprili 2009

Wanamgambo wa Taleban waondoka katika eneo la Buner nchini Pakistan

https://p.dw.com/p/HdFN
Waziri mkuu wa Pakistan Yousaf Raza Gilani.Picha: AP

Waziri mkuu wa pakistan Yousuf Raza Gilani amewaonya wanamgambo wa Taliban kuwa serikali itawachukulia hatua ikiwa watakiuka maelewano waliyoafikiana ambapo serikali ilikubali kutumika kwa sheria za kiislamu katika wilaya ya Malakand inayolijumuisha eneo la swat.

Onyo hilo linatolewa huku marekani ikiendelea kuishinikiza Pakistan , taifa lililo na nguvu za nuklia kukabiliana na wanamgambo hao wa Taliban wanaoendelea kuyadhibiti maeneo zaidi.

Wanamgambo wa Taleban wanaolidhibiti eneo la kaskazini magharibi mwa Pakistan la Buner wanatarajiwa kuondoka katika eneo hilo baadaye hii leo kulingana na taarifa iliyotolewa na msemaji wa wanamgambo hao.

Wiki iliyopita rais wa pakistan Asif Ali Zardari aliidhinisha kutumika kwa sheria za kiislamu , sharia, katika eneo la kaskazini magharibi mwa pakistan, miezi miwili baada ya makubaliano kati ya wanamgambo wa Taliban na serikali.

Katika maelewano hayo serikali ya pakistan ilikubali kuweka mahakama za kiislamu katika eneo la swat, ili kumaliza mashambulizi yaliyodumu kwa miezi kadhaa, yaliyofanywa na wanamgambo wa Taliban na ambapo mamia ya watu waliuawa.

Akiliutubia bunge hii leo, waziri mkuu wa pakistan Yousuf Raza Gilani aliapa kuwa watawachukulia hatua wanamgambo hao ikiwa makubaliano yaliyoafikiwa yatakiukwa.

Taliban, Archivbild
Wapiganaji wa Taliban nchini PakistanPicha: picture-alliance/dpa

Wiki hii wanamgambo wa Taliban walisonga mbele kutoka ngome yao hadi wilaya ya Buner iliyo umbali wa kilomita 100 kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa Pakistan Islamabad.

Hata hivyo msemaji wa kamanda wa wanamgambo wa Taliban nchini Pakistan alisema kuwa kamanda wa wanamgambo hao aliwaamrisha wapiganaji hao kuondoka katika wilaya waliyoiteka ya Buner.

Muslim Khan alisema kuwa karibu wanamgambo 100 wa Taliban walikuwa katika wilaya ya Buner.Khan alisema kuwa wawakilishi wa serikali pamoja na wa wanamgambo wa Taliban wataelekea katika eneo la Buner kupeleka ujumbe wa kuwataka wanamgambo hao kuondoka.

Wiki iliyopíta Khan alinukuliwa akisema kuwa mtandao wa al Qaeda utapata mazingira salama katika maeneo yaliyo chini ya wanamgambo wa Taleban.

Tangazo hili linakuja huku marekani ikisema kuwa inatathmini hali katika eneo la Buner ambapo wanamgambo wa Taleban waliojihami wamekuwa wakipiga doria kwa siku tatu mfululizo.

Wanamgambo hao waliweka vizuizi vya barabarani na kuidhibiti misikiti huku wakiwaonya wakazi kutoendesha shughuli zinazoenda kinyume na sheria za kiislamu na pia kuweka marufu ya wanawake kutoonekana hadharani

Hapo Awali waziri wa masuala ya kigeni wa marekani Hillary Clinton alitoa tahadhari kuwa Pakistan inelekea kuwa tisho kwa usalama wa duniani, matamshi ambayo yalikanushwa na Pakistan iliyosema kuwa inakabilina vilivyo na makundi yenye itikadi kali pamoja na Ugaidi.

Mwandishi: Jason Nyakundi

Mhariri: Ramadhani Yusuf Saumu