1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pakistan yatumbukia zaidi katika mzozo wa kisiasa

7 Novemba 2007

Bunge nchini Pakistan limeidhinisha hali ya hatari iliyotangazwa na rais Pervez Musharraf na wakati huo mamia ya wafuasi wa waziri wa zamani Benazir Bhutto wametimuliwa na polisi muda mfupi baada ya kiongozi huyo kuitisha maandamano kupinga amri ya rais Musharraf.

https://p.dw.com/p/C779
Jemedari Pervez Musharraf
Jemedari Pervez MusharrafPicha: picture-alliance/dpa

Hali nchini Pakistan inazidi kutumbukia katika mzozo wa kisiasa muda mfupi uliopita waziri mkuu wa zamani Benazir Bhutto ametangaza kuwa amekatisha uhusiano wake na rais Pervez Musharraf.

Polisi mjini Islamabad wametumia gesi ya kutoa machozi kuwatawanya wafuasi wa bibi Benazir Bhutto muda mfupi tu kiongozi huyo wa upinzani alipoitisha maandamano kupinga amri ya hali ya hatari iliyotangazwa na rais Pervez Musharraf.

Takriban wafuasi 200 wa bibi Benazir Bhutto walikuwa wamekusanyika ili kuanza masafara kulelekea kwenye majengo ya bunge huku wakiimba nyimbo za kulaani amri ya hali ya hatari.

Televisheni ya taifa imetangza kwamba bunge nchini Pakistan limeidhinisha rasmi amri ya hali hiyo ya hatari liyotolewa na rais Pervez Musharraf.

Bibi Bhutto ametishia kuwa ataongoza maandamano makubwa katika mji mkuu wa Islamabad iwapo rais Pervez Musharraf hata achia madaraka ya kijeshi ameapa kuwa ataendelea na maandamano ya siku ya ijumaa katika mji wa Rawalpindi licha ya vitisho vya polisi kwamba watayavunja maandamano hayo.

Waziri huyo mkuu wa zamani wa Pakistan amesema kuwa rais Musharraf lazima aieheshimu katiba na atangaze tarehe ya kufanyika uchaguzi wa mwezi januari mwakani.

Bibi Benazir Bhutto amesisitiza kuwa rais Pervez Musharraf atimize ahadi alizozitoa mbele ya taifa.

Wakati huo huo waziri mkuu mwingine wa zamani Nawaz Sharrif amezitolea mwito nchi za magharibi zimtenge kiongozi wa kijeshi wa Pakistan jenerali Pervez Musharraf.

Sharif amezungumza hayo akiwa nchini Saudi Arabia alikorejeshwa mara tu alipojaribu kurejea nchini Pakistan, amesema kuwa nchi za magharibi zisipochukua hatua hiyo ya kumtenga rais Musharraf basi Pakistan itatumbukia zaidi kwenye mzozo.

Mjini Islamabad seriklali imekosoa shinikizo za jamii ya kimataifa dhidi ya amri ya hali ya hatari iliyotangazwa na rais Pervez Musharraf.

Wizara ya mambo ya nje ya Pakistan imesema kuwa imesikitishwa na nchi za kigeni jinsi zinavyo laani hali ya hatari iliyotangazwa nchini Pakistan kana kwamba hazielewi hali ngumu inayoikumba nchi hiyo.

Marekani na Uingereza zimeungwa mkono na nchi 27 wanachama wa umoja wa ulaya katika kumtaka rais Musharraf awaachie wafungwa wa kisiasa wakiwemo wanasheria, alegeze sheria kali dhidi ya vyombo vya habari na pia atafute maelewano na upande wa upinzani.

Nchi 53 zilizokuwa chini ya utawala wa Uingereza zimetisha mkutano wa mawaziri katika mji wa London wiki ijayo kujadili hali ya Pakistan.