1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pande hasimu zakutana kwa mazungumzo Geneva

Angela Mdungu
26 Februari 2020

Mahasimu wa kisiasa wa Libya wamekutana leo Jumatano 26.02.2020 katika mazungumzo chini ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva. Mazungumzo hayo yalilenga kumaliza awamu mpya ya mapigano katika mji mkuu wa Libya, Tripoli

https://p.dw.com/p/3YTYi
Bildkombo Haftar und as-Sarradsch

Kuanza kwa mazungumzo ya usuluhishi ambako ni moja ya njia za utatuzi wa migogoro zinazotumiwa na umoja wa mataifa kumetokana na  makubaliano yaliyofanyika wiki hii kati ya maafisa wa jeshi ili amri ya kuweka chini silaha ianze kazi  rasmi  hali ambayo bado inasuasua mjini Tripoli.

Makubaliano yaliyotangazwa ya kuweka chini silaha ambayo kwa sasa yanapitiwa na viongozi wawili wanaokinzana yanazungumzia kurejea kwa maelfu ya raia waliolazimika kuyakimbia makazi yao katika mji mkuu Tripoli. Hata hivyo makubaliano hayo hayataji mambo muhimu yanayoleta ubishi kwenye mzozo huo, kama vile kuwaondoa wanajeshi walio mashariki mwa Libya au kuwaondoa wanamgambo wenye mahusiano na serikali ya Tripoli inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Hata hivyo waziri wa mambo ya kigeni wa serikli ya Haftar, Abdulhadi Lahweej akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva hata hivyo ameituhumu serikali ya Uturuki kuingilia mgogoro wa nchi hiyo.

Mazungumzo yanayokwama licha ya mataifa yenye nguvu kuhusishwa katika usuluhishi

Mazungumzo ya kutafuta amani yamekuwa yakisita katika wiki mbili zilizopita wakati fujo za  kiwango cha chini zikiendelea katika mji huo na silaha zikimiminika katika nchi hiyo iliyochakazwa na vita licha ya mataifa yenye nguvu duniani kuahidi kusaidia juhudi za kutuliza hali walipokutana mjini Berlin mwezi uliopita.

Libyen Khalifa Haftar
Jenerali Khalifa HaftarPicha: AFP/A. Doma

Kamanda wa vikosi vya Mashariki mwa nchi hiyo Khalifa Khaftar na wafuasi wake ambao wanadhibiti maeneo ya mashariki na kusini mwa Libya, walianzisha mashambulizi ya kutaka kuudhibiti mji mkuu Tripoli Mwezi Aprili mwaka uliopita. Mapambano hayo yamesababisha mauaji ya wa mamia ya watu na zaidi ya raia 150,000 wamelazimika kuyakimbia makazi yao.

Haftar anaungwa mkono na Misri, Falme za kiarabu, Urusi pamoja na Ufaransa. Serikali ya Libya inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa imekuwa ikiitegemea Uturuki kwa misaada ya kijeshi ikiwemo ulinzi wa anga na wapiganaji walio karibu na Syria kusaidia kukabiliana na wapiganaji wa Haftar.

Hayo yanaendelea wakati shrika la habari la Interfax likiripoti kuwa Urusi hii leo imeituhumu Uturuki kuwasaidia wapiganaji wa kigeni kuingia Libya.