1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pande zinazozana Yemen zakubaliana kubadilishana wafungwa

Caro Robi
6 Desemba 2018

 Pande zinazozana Yemen zimekubaliana kuwaachia huru maelfu ya wafungwa katika kile mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths alichokitaja kuwa mwanzo wenye matumaini wa mazungumzo ya kwanza ya kutafuta amani.

https://p.dw.com/p/39am7
Schweden Friedensgespräche für Jemen starten vor Drohkulisse
Picha: Reuters/TT News Agency/S. Stjernkvist

Griffiths amewaambia waandishi wa habari kuwa hatua ya kuwaleta wajumbe wa serikali na kundi la waasi wa Houthi katika meza ya mazungumzo ni hatua muhimu.

Tangu mwaka 2016, pande hizo mbili zinazozana hazijakaa pamoja kwa mazungumzo kuvimaliza vita vya karibu miaka minne ambavyo vimesababisha mamilioni ya watu kukumbwa na baa baya zaidi  la njaa ulimwenguni.

Griffiths amesema makubaliano yaliyofikiwa leo ya kubadilishana wafungwa yatasaidia katika kuunganisha maelfu ya familia.

Martin Griffiths UN Sonderbeauftragter Jemen
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Yemen Martin GriffithsPicha: picture-alliance/Keystone/S. Di Nolfi

Je, ni ukurasa mpya kwa Yemen?

Shirika la Msalaba mwekundu limesema takriban wafungwa 5,000 wataachiwa huru. Duru za Umoja wa Mataifa zimearifu kuwa wanadiplomasia wanatarajiwa kushauriana na pande hizo mbili zinazozana kujadili hatua nyingine za kupunguza uhasama na kuundwa kwa serikali ya mpito.

Inaripotiwa wajumbe wa serikali ya Yemen na waasi wa Houthi bado wako mbali kufikiana kuhusu masuala muhimu, yakiwemo nani atadhibiti bandari ya Hodeida na iwapo waasi wanapaswa kuondoka kabisa kutoka mji wa Hodeida.

Umoja wa Mataifa unajaribu kuepusha mapigano makubwa katika mji huo wa bandari muhimu ambayo inatumika pakubwa kuingiza bidhaa nchini Yemen.

Waasi wa Houthi pia wanaudhibiti mji mkuu Sanaa, ambapo muungano wa majeshi yanayoongozwa na Saudi Arabia yanadhibiti uwanja wa ndege wa Sanaa.

Baa la njaa lazidi

Waziri wa mambo ya nje wa Yemen Khaled al Yamani ambaye anaoungoza ujumbe wa serikali amesema upande wake utazingatia mpango wa kubadilishana wafungwa na waasi wa Houthi lakini wanatofautiana kuhusu mji muhimu wa bandari wa Hodeida.

Jemen Konflikte
Mtoto anayeteseka kutokana na utapiamlo YemenPicha: Getty Images/AFP/E. Ahmed

Yamani amesema Wahouthi sharti waondoke mjini Hodeida na bandarini na kuukabidhi kwa serikali halali.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya  Yemen vimesababisha vifo vya takriban watu 10,000 na kusababisha mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu ambapo watu milioni 14 wanakabiliwa na baa la njaa.

Nalo shirika la mpango wa chakula duniani WFP limesema zaidi ya watu milioni 15 nchini Yemen wanakabiliwa na hali za dharura za baa la njaa na idadi hiyo huenda ikaongezeka hadi milioni 20.

WFP imesema inapanga kuongeza utoaji wa misaada ya chakula kuwasaidia zaidi ya watu milioni nne zaidi nchini humo ifikapo mwisho wa mwezi Januari na hivyo kuwafikia Wayemeni milioni 12 wanaohitaji kwa dharura msaada wa chakula.

Miongoni mwa ni wanawake na watoto milioni tatu wanaohitaji msaada maalum kutibu na kuepusha utapiamlo mbaya.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/afp

Mhariri: Yusuf Saumu