1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Benedicto wa XVI azisihi dini kushikamana

Nijimbere, Gregoire18 Julai 2008

Kiongozi wa kanisa la kikatoliki duniani Baba Mtakatifu Benedicto wa XVI, ametoa mwito wa kuondoa tofauti kati ya dini na kuheshimu binaadamu ambae ni kiumbe cha Mungu.

https://p.dw.com/p/Eeiz
Baba Mtakatifu Benedicto wa XVI akiwa Sydney AustraliaPicha: picture-alliance/dpa

Katika sherehe hizo zinazoendelea mjini Sydney Australia kuhusiana na Siku Kuu ya Vijana Duniani, waumini zaidi ya laki mbili wengi wao vijana wamefanya kile kilichotajwa ´´Safari ya Msalaba´´ mjini Sydney ambayo inaigiza vipi Mtume Yesu Kristu alivyoandamwa hadi kusulubiwa. mwenyewe akikubali hayo yote kutuokoa. Na kitendo hicho kimeigizwa na wataalamu wa michezo ya kuigiza.

Baada ya safari hiyo, Baba Mtakatifu Benedicto wa XVI ameanza kuwahotubia waumini akisema hii ni fursa nyingine kuwasihi waumini wa dini zote kuzidi kushikamana na kuwa kitu kimoja badala ya kutilia mbele tofauti. Kwani amezidi kuelezea kwamba kimsingi hakuna tofauti kwani Mungu ni moja ila sala ndizo zatofautiana.

Kwa hiyo baadhi ya watu licha ya kuwa waumini, wanahitaji kurekebisha mwenendo wao . Kuhusu jambo hilo, Papa Benedicto wa XVI amezidi kushauri: ´´Ndugu zangu. Kiumbe cha Mungu ni kimoja na ni kizuri. Kinahitaji tu utulivu, maendeleo, amani na mazingira mazuri. Na ndio sababu haieleweki hata kidogo uharibifu wowote dhidi ya binaadamu kwa kumuendea kinyume na vile alivyoumbwa´´.

Sherehe kuhusiana na Siku Kuu ya Vijana Duniani zimeingia leo siku ya tano ambapo zinatarajiwa kuhitimishwa jumapili wiki hii. Kuna uwezekano kwamba katika hotuba yake ya kesho Baba Mtakatifu akaomba tena radhi kuhusu ukatili wa ngono ambapo baadhi ya mapadri walihusika wakiwemo hata mapadri wa hapo mjini Sydney. Na kama kawaida yake, na kabla ya kuanza shughuli, Baba mtakatifu ameanza kuwapokea kwa mazungumzo viongozi wa kanisa nyingine za kikristu na dini nyingine. Amekiri kuwa kuna matatizo siku hizi juu ya uhusiano kati ya dini ambao uongozi wa kanisa la kikatoliki mjini Vatican Roma Italy umeanza kuushughulikia kwa jitihada zote.