1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis ahubiri amani na uadilifu Kenya

26 Novemba 2015

Kiongozi wa kanisa Katoliki ulimwenguni Papa Francis ameanza ziara yake ya kihistoria barani Afrika akiwa na ujumbe wa wazi kwa viongozi wa Kenya: vita dhidi ya rushwa na umaskini

https://p.dw.com/p/1HCiV
Kenia Papst Franziskus in Nairobi
Picha: Getty Images/AFP/G. Cacace

Papa Francis bila shaka alikuwa na haraka kuanza ziara yake ya kwanza barani Afrika. Dege iliyombeba ilitua katika uwanja wa ndege wa kimataifa mjini Nairobi dakika chache kabla ya muda uliopangwa. Alionekana mwenye utulivu na tabasamu na kuwapungia mkono watumbuizaji wa nyimbo za kitamaduni, waliokaribisha kwa kuimba “karibu Kenya Papa”. Rais Uhuru Kenyatta, ambaye ni mkatoliki aliongoza umati wa viongozi wa kisiasa na kidini waliofika kumkaribisha Papa uwanjani humo.

Kiogozi huyo wa kanisa katoliki alitumia hotuba yake katika Ikulu ya Rais kwa kutoa ujumbe wa wazi kwa wanasiasa wa Kenya. “ninawahimiza mfanye kazi kwa uadilifu na uwazi ili kuiboresha jamii” alisema. Pia aliwataka wanasiasa kuwajali maskini.

Kenia, Papst Franziskus besucht Kenia
Papa Francis akiwasili mjini NairobiPicha: Reuters/G. Tomasevic

Papa Francis pia alisisitiza kuhusu mada nyingine mbili muhimu: umaskini na mazingira. “uzoefu unaonyesha kuwa machafuko, migogoro na ugaidi hutokana na hofu, kutoelewana na kukata tamaa mambo yanayosababishwa na umaskini na masikitiko” alisema Papa. Alitoan wito kwa jamii ya kimataifa kuimarisha juhudi za kulinda mazingira, akionya kuwa mgogoro mkubwa wa kimazingira unaukabili ulimwengu. Wakati huo huo, alisifu heshima ya kitamaduni kwa mazingira katika jamii nyingi za kiafrika. “Kenya ina utamaduni wa kuhifadhi ambao unawapa heshima”. Alisema.

Rais wa Kenya aahidi kupambana na rushwa

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akionekana mnyenyekevu, katika hotuba yake ya kumkaribisha Papa. “ni heshima kwetu, na fahari kubwa kuwa ulichagua kuanzia safari yako barani Afrika, hapa Kenya.” Alimwambia Baba Mtakatifu.

Kenyatta alimwomba Papa Francis kumwombea katika vita dhidi ya rushwa. “katika moyo wa kila mkenya tunafahamu kuwa tunastahili kushinda vita hivi na ni jukumu langu kuongoza vita hivyo”. Alisema. Pia alisisitiza ziara ya Papa kuwa fursa kwa Kenya kumaliza migawanyiko ya kikabila na kidini.

Kenia Papst Franziskus & Uhuru Kenyatta
Papa Francis aliandaliwa gwaride la heshimaPicha: Reuters/S. Rellandini

Usalama mkali

Usalama umeimarishwa mjini Nairobi kabla ya misa ya leo. Zaidi ya polisi 10,000 na wanachama 10,000 wa Huduma ya Vijana kwa Taifa wamewekwa katika maeneo ya mjini humo. Kwa sababu za kiusalama, barabara kuu zinazoingia na kutoka katikati ya mji wa Nairobi zitasalia kufungwa. Zaidi ya watu milioni 1.4 wanatarajiwa kuhudhuria misa itakayoandaliwa katika Chuo Kikuu cha Nairobi.

Akiwa kwenye ndege kuelekea Kenya, Papa Francis mwenye umri wa miaka 78 alipuuza wasiwasi kuhusu ziara yake nchini Kenya na Uganda. Nchi zote mbili zimewahi kulengwa na mashambulizi ya wanamgambo wa al-Shabaab. Lakini aliwaambia waandishi wa habari kuwa “kusema ukweli, kitu tu kinachonipa wasiwasi ni mbu”.

Hii leo atakutana na viongozi kadhaa nchini humo, wakiwemo maaskofu na wahubiri, na pia kukitembelea kitongoji cha Kangemi. Pia atawahutubia vijana katika sherehe maalumu kesho Ijumaa kabla ya kuelekea Uganda

Mwandishi: Daniel Pelz/DW
Tafsiri: Bruce Amani
Mhariri: Josephat Charo