1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis akamilisha ziara Uturuki

30 Novemba 2014

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis amekamilisha ziara yake nchini Uturiki kwa kushiriki ibada maalum katika kanisa la Kiodhodox iliyoongozwa na kiongozi wa kanisa hilo Bartholomew wa kwanza.

https://p.dw.com/p/1DxFr
Papa Francis akikumbatiwa na kiongozi wa Orthodox Bathelomew wa kwanza
Papa Francis akikumbatiwa na kiongozi wa Orthodox Bathelomew wa kwanzaPicha: Reuters/U.Bektas

.Papa Francis amekamilisha ziara hiyo kwa kuchukua hatua ya kuonyesha kuwakaribia zaidi waislamu pamoja na wakristo wa madhehebu mengine.

Kushiriki kwa kiongozi huyo wa wakatoliki duniani katika ibada kwenye kanisa la Orthodox la mtakatifu George lililoko mjini Istanbul ilikuwa mojawapo ya ishara mpya kabisa ya kuimarika kwa uhusiano kati ya kanisa Katoliki na makanisa ya Orthodox chini ya papa Francis.

Papa akihudhuria ibada katika kanisa la Orthodox,Istanbul
Papa akihudhuria ibada katika kanisa la Orthodox,IstanbulPicha: Reuters/T.Gentile

Ikumbukwe kwamba Jumamosi kiongozi huyo wa kidini alifanya ziara katika msikiti wa Sultan Ahmet unaojulikana kimataifa kama msikiti wa Buluu alisimama upande wa kibla au Mecca katika membari ya msikiti huo kwa muda wa dakika mbili akiwa pamoja na kiongozi wa juu wa dini ya kiislamu nchini Uturuki.

Halikadhalika siku hiyo ya Jumamosi jioni aliinamisha kichwa chake na kumuomba kiongozi wa kanisa la Orthodox,Batholomew kumbusu kwenye paji lake la uso kama ishara muhimu ya huruma kuelekea kiongozi huyo wa Othodox.Papa na Batholomew wamekuwa wakishirikiana katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita kuelekea maridhianao kati ya makanisa ya eneo la mashariki na magharibi ambayo yamegawika tangu mifarakano ya mwaka 1054.

Kukutana kwa viongozi hao wawili wa imani ya kikristo ni hatua ya hivi karibuni kabisa muhimu katika kukurubia mchakato wa maridhiano ulioanzishwa mwaka 1964 na papa Paul VI na kiongozi wa kanisa la Orthodox wakati huo Atnenagoras ukiwa ni mkutano wa kwanza wa aina yake tangu karne 15.

Papa Francis ametia saini azimio la pamoja na Batholomew ambaye cheo chake kamili ni Askofu mkuu wa Constantinople,New Rome na Ecumenical Patriarch kabla ya kurudi mjini Roma.Bartholomew ambaye ni kiongozi anayepewa heshima kubwa hadi nje ya kanisa la Kiodhodox anaongoza kanisa la Orthodox katika wadhifa ambao umeanzia tangu mwanzoni mwa utawala wa Byzantine zaidi ya milenia moja iliyopita kabla ya Ottoman kuidhibitI Constantilope mwaka 1453.

Papa akikaribishwa na Mufti wa Istanbul Rahmi Yaran nje ya msikiti wa Sultan Ahmet
Papa akikaribishwa na Mufti wa Istanbul Rahmi Yaran nje ya msikiti wa Sultan AhmetPicha: Reuters/O.Orsal

Makazi ya Patriarchate mjini Istanbul ndio makao makuu ya kiongozi wa kanisa hilo la Ordhodox na kwa mujibu wa sheria za Uturuki kiongozi wa kanisa hilo analazimika kuwa raia wa nchi hiyo.Ziara ya siku tatu ya papa Francis nchini Uturuki imejumuisha pia mazungumzo na rais wa taifa hilo Recep Tayyip Erdogan mjini Ankara ambapo kiongozi huyo alitowa mwito wa kufanyika mdahalo kati ya dini na imani mbali mbali kumaliza tatizo la itikadi kali.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Mohammed Dahman