1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ni mkutano wa kihistoria baina ya madhebehu mawili

Sylvia Mwehozi23 Mei 2016

Kiongozi mkuu wa kanisa katoliki duniani Papa Francis amekutana na kufanya mazungumzo na Imam mkuu wa msikiti wa Al-Azahr wa nchini Misri ikiwa ni ishara nzuri ya mahusiano baina ya dini mbili.

https://p.dw.com/p/1ItCU
Vatikan Papst Franziskus empfängt Großimam aus Kairo
Picha: Reuters/M. Rossi

Kiongozi mkuu wa kanisa katoliki duniani Papa Francis amekutana na kufanya mazungumzo na Imam mkuu wa msikiti wa Al-Azahr wa nchini Misri ikiwa ni ishara nzuri ya mahusiano baina ya dini mbili. Mkutano huu unatajwa kuwa wa kwanza na wa kihistoria baina ya kiongozi huyo wa kanisa katoliki na kiongozi wa juu wa kiislamu.

Mahusiano baina ya kituo hicho cha Al-Azhar kinachotoa mafunzo ya kiislamu nchini Misri na Vatican yalikatika mwaka 2011 wakati ambapo kiongozi wa kanisa katoliki wa wakati huo Benedict wa 16 alipotajwa kurudia kuikashifu dini ya kiislamu.

Uamuzi huo ulikuja baada ya kauli ya Papa Benedict ya kusema kulikuwa na "mkakati wa vurugu uliowalenga wakristo" baada ya watu 23 kuuawa katika shambulizi la bomu lililotekelzwa nje ya kanisa mjini Alexandria nchini Misri.

Tangu kuchaguliwa kwake mwaka 2013, Papa Francis ameweka mkazo katika kuboresha mahusiano baina ya imani zote . Ameonekana mwenye furaha wakati alipomsalimia kiongozi huyo Ahmed al-Tayeb.

Abbas Shuman , naibu imam mkuu ameliambia shirika la habari la AFP jana kwamba ishara anazotoa Papa Francis kwa Waislamu zimemshawishi Tayeb kukutana nae.

Papa Francis amewaambia waandishi wa habari kuwa "mkutano wetu ni ujumbe ".

Katika tamko juu ya ziara ya Imam huyo, wanasema Sheikh Tayeb amekubali kukutana na Papa Francis katika jitihada zake za kuendeleza amani.

Papa Francis akifanya mazungumzo na Imam Ahmed Al-Tayeb mjni Vatican
Papa Francis akifanya mazungumzo na Imam Ahmed Al-Tayeb mjni VaticanPicha: Getty Images/AFP/M. Rossi

Katika kauli iliyotolewa na Vatican, inasema viongozi hao pia wamejadili juu ya matatizo ya ugaidi na machafuko pamoja na hali ya wakristo walioko mashariki ya kati na namna nzuri ya kuwalinda.

Kuonyesha mfano kwa mataifa ya magharibi , Papa Francis amewapokea baadhi ya wakimbizi waliokimbia vita nchini Syria. Wiki iliyopita pia aliyashuku mataifa ya magharibi kwa kutaka kuiuza aina yao ya demokrasia katika mataifa ya Afrika na Mashariki ya kati pasipo kuzingatia siasa za ndani.

Mwaka jana Papa Francis alitoa rai ya kukomeshwa kile alichokiita kuwa mauaji ya kimbari ya wakristo katika eneo la mashariki ya kati ingawa alionya kwamba haikuwa sahihi kuwahusisha waislamu na machafuko.

Wakristo wa madhehebu ya koptiki ni asilimia 10 ya wakazi wote wa Misri ambapo idadi kubwa ni waislamu wa madhebu ya sunni.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/Reuters

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman