1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa aongoza Misa ya Kihistoria katika Rasi ya Uarabuni

Grace Kabogo
5 Februari 2019

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis leo ameadhimisha ibada ya Misa katika Umoja wa Falme za Kiarabu iliyohudhuriwa na maelfu ya watu.

https://p.dw.com/p/3Cj2m
VAE Papst Franziskus - Messe in Abu Dhabi
Picha: Reuters/T. Gentile

Hiyo ni ibada kubwa ya kwanza ya kipapa kufanyika katika Rasi ya Uarabuni, ambako ndiko alikozaliwa Mtume wa mwisho wa Waislamu.

Kiasi cha watu 135,000 wamehudhuria ibada hiyo ya Misa katika uwanja wa michezo wa Zayed kwenye mji wa Abu Dhabi. Kwa mujibu wa duru za Kanisa Katoliki, waliohudhuria ni Wakatoliki kutoka mataifa 100 pamoja na Waislamu wapatao 4,000, wakiwemo viongozi wa serikali.

Ibada hiyo imefanyika siku moja baada ya Papa Francis kutoa wito kwa viongozi wa Kikristo na Kiislamu kushirikiana kwa kiasi kikubwa kuimarisha amani na kukataa vita, pamoja na kuruhusu uhuru wa kidini.

VAE Papst Franziskus in Abu Dhabi
Papa Francis akiwasili kwenye uwanja wa michezo wa Zeyed, Abu DhabiPicha: Reuters/A. Jadallah

''Uhuru ni haki ya kila mwanadamu. Kila mtu anapaswa kufurahia uhuru wa imani, mawazo na matendo yake. Tofauti za kidini, rangi, jinsia au lugha zilitokana na mapenzi ya Mungu ambaye aliwaumba binaadamu wote. Hekima hii ni chanzo cha haki ya kuwa huru kuabudu na uhuru wa kuwa tofauti,'' alisema Papa Francis.

Umoja wa Falme za Kiarabu ni nchi ya Kiislamu, ambako kuna idadi kubwa ya wahamiaji hasa kutoka barani Asia. Vatican imekadiria kuwa kuna kiasi ya Wakatoliki 900,000 nchini humo. Huku Wakristo wakiruhusiwa kuabudu katika imani yao kwenye Umoja wa Falme za Kiarabu, jambo hilo halifanyiki taifa jirani la Saudi Arabia, ambako hairuhusiwi kujenga makanisa.

Papa awataka viongozi kulaani ghasia 

Baba Mtakatifu pia amelaani vikali ghasia zinazofanywa kwa kutumia jina la dini na amewasihi viongozi wa kidini kukemea mifumo yote ya ghasia bila kusita.

Katika ibada hiyo nyimbo za ''Halleluja'' ndiyo zilikuwa zinasikika na hivyo kuweka alama ya kihistoria na kuonesha ushahidi kwamba Umoja wa Falme za Kiarabu kweli unazingatia suala la uvumilivu wa imani na dini nyingine.

Papst Franziskus in Abu Dhabi
Papa Francis akisalimiana na viongozi wa Umoja wa Falme za KiarabuPicha: Reuters/A. Jadallah

Shangwe zilisikika ndani na nje ya uwanja huo wa michezo wakati Papa Francis alipowasili na kupita pembeni ya umati wa watu akiwa kwenye gari la wazi la Kipapa, huku watu wakitamka maneno ya kumsalimu Papa kama vile ''Viva Papa'' na ''Tunakupenda Papa''.

Papa Francis jana aliuzuru Msikiti Mkubwa, akiwa ameongozana na Ahmed al-Tayyeb, Imam wa Al-Azhar, chuo kikuu maarufu cha Waislamu wa madhehebu ya Sunni nchini Misri. Papa Francis aliyewasili siku ya Jumapili katika Umoja wa Falme za Kiarabu kutokana na mwaliko alioupata kutoka kwa mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo, Mohamed bin Zayed Al Nahyan anaikamilisha ziara yake hii leo.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPA, AP, AFP, Reuters
Mhariri: Mohammed Khelef