1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Papa Francis apokelewa kwa shangwe Ufilipino

Admin.WagnerD15 Januari 2015

Kiongozi wa kanisa Katoliki Duniani Papa Francis , amekaribishwa kwa ngoma na muziki na waaumini , kwa lengo la kuanza ziara ya siku tano katika taifa hilo la Asia lenye idadi kubwa ya Wakatoliki.

https://p.dw.com/p/1ELHT
Papst Ankunft in Manila 15.01.2015
Picha: picture-alliance/dpa/D. M. Sabangan

Milio ya kengele ilisikika katika maeneo yote ya taifa hilo wakati ndege ya shirika la Ndege la Sri Lanka,iliyomsafiosha kiongozi huyo wa kanisa katoliki, Muargentina mwenye umri wa miaka 78 ilipotua katika uwanja wa ndege wa Villamor mjini Manila.

Rais wa Ufilipino Benigno Aquino (Akino) aliongoza serikali na maafisa wa kanisa katoliki kumkaribisha Papa Francis.Rais Aquino aliibusu pete ya Papa akizungumza naye kabla ya kumkabidhi maua.


Inakadiriwa kiasi ya watoto yatima 1,200 walicheza ngoma katika eneo la lami la uwanja huo. Papa alioneshwa kuvutiwa na watoto yatima wawili Lanie Ortillo mwenye umri wa miaka tisa na Mark Angelo Balbero, aliyekuwa na umri wa miaka kumi aliwabariki katika eneo hilo kabla ya kukutana na maafisa.

Katika hafla hiyo ya mapokezi mtoto Ortillo alimwambia papa na hapa namnukuu „ Bievenido Papa Francisco akimaanisha karibu sana Papa francis. Tafadhali waombee Wafilipino“ mwisho wa kumnukuu. Mtoto huyo yatima aliyasema hayo wakati akimkabidhi mauwa.

Straßenszene in Manila Philippinen - Besuch Papst Franziskus
Picha ya Papa Francis mitaa ya ManilaPicha: asd/F.R. Malasig

Umati mkubwa ulijipanga nje ya kambi hiyo ya jeshi la anga kumlaki kiongozi huyo huku wakipeperusha vibendera vidogo vya rangi ya njano na nyeupe au vitambaa vya mkononi, wakati msafara wake ukipita kuelekea katika eneo ambalo litakuwa makazi yake katika kipindi hiki cha ziara yake nchini humo.

Papa alionekana akitabasamu wakati wote akiupungia mkono umati .ambapo wengi wao walikuwa wakipiga picha na simu zao za mkononi na kububujikwa na machozi. Maneno yaliyokuwa yakisika kwa wakati huo kwa lugha ya Kifilipino yalikuwa „ Pope Francis Mabuhay“ ikiwa na maana karibu Papa Francis .

Philippinen President Benigno Aquino
Rais wa Ufilipino Benigno AquinoPicha: Jay Directo/AFP/Getty Images

Mkusanyiko wa kumpokea Papa ulianza mapema asubuhi ya leo ulikuwa wa umbali wa kilometa 22. Waumini walipeperusha viashiria vya kumkaribisha Papa na kufanya ibada za kimya kimya huku mwanafunzi mmoja wa kike aliyejulikana kama Catherine akionekana mwenye furaha kumuona papa Francis nchini mwao.

Serikali ya Ufipino ilifunga barabara kadhaa kutoka uwanja wa ndege na kutangaza amri ya kutoruka ndege katika eneo la Manila. Karibu maafisa wa polisi 40,000, wanajeshi na askari wa usalama barabarani walisambazwa mitaani kutokana na ujio huo, ambao vile vile utamfikisha Papa Francis katika mji wa mashariki wa Tacloban, ambako kimbunga Haiyan kilisababisha vifo vya watu zaidi ya 6,300 mwaka 2013. papa aliwasili Ufilipino baada ya ziara yake nchini Sri Lanka.

Mwandishi:Nyamiti Kayora/DPE

Mhariri:Mohamed Abdul Rahaman