1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

PARIS: Condoleezza Rice akutana na Fouad Siniora

26 Juni 2007
https://p.dw.com/p/CBoB

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani, Condoleezza Rice, amekutana mapema leo na waziri mkuu wa Lebanon, Fouad Siniora, mjini Paris, Ufaransa.

Mkutano huo unalenga kumuunga mkono waziri mkuu Siniora na serakali yake huku kukiwa na mapigano na hali ya wasiwasi ikitanda katika eneo la kaskazini mwa Lebanon kwa sababu ya ushawishi wa Syria.

Waziri Condoleeza Rice anatarajiwa kukutana na rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy baadaye leo. Bi Rice yumo mjini Paris kwa mazungmuzo ya kwanza na rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, tangu rais huyo aliposhinda uchaguzi mwezi uliopita.

Mkutano wa leo unafanyika baada ya wanajeshi sita wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kuuwawa kwenye shambulio la bomu la kutegwa ndani ya gari kusini mwa Lebanon juzi Jumapili.

Jana usiku waziri Condoleezza Rice alisisitiza umuhimu wa juhudi za Umoja wa Mataifa kuunda tume maalumu itakayosikiliza kesi za washukiwa waliohusika na mauaji ya waziri mkuu wa zamani wa Lebanon, Rafik Hariri.