1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Patashika Guinee-Bissau

Oumilkher Hamidou3 Machi 2009

Walimwengu wadai katiba iheshimiwe Guinee Bissau

https://p.dw.com/p/H4aM
Rais Nino Vieira wa Guinee BissauPicha: picture-alliance/ dpa


Rais Joao Bernardo Vieira wa Guinea Bissau ameuliwa na wanajeshi, muda mfupi baada ya kuuliwa mkuu wa vikosi vya wanajeshi na kuitumbukiza katika bahari ya mrafaruku nchi hiyo ndogo na maskini ya Afrika Magharibi ambayo tokea hapo imedhoofishwa kwa biashara ya madawa ya kulevya.


Kufuatia laana na miito ya jumuia ya kimataifa ya kutaka hali ya utulivu, ,jeshi la Guinea Bissau limesema hakujatokea mapinduzi na kuahidi kuheshimu katiba.


Hali inasemekana ni shuwari katika mji mkuu, Bissau.Vikosi vya kiijeshi vimewekwa katika maeneo muhimu ya mji mkuu huo.


Rais Vieiera alipigwa risasi na kufa,alfajiri ya jana,kufuatia shambulio la bomu la hapo awali, lililogharimu maisha ya jenerali Batista Tagmé Na Waié katika makao makuu ya jeshi.


Mashambulio hayo mawili yamezusha hali ya mtafaruku.


"Hali inatatanisha bado,yadhihirika yote haya yameandaliwa na jeshi. Ni mapinduzi haya", alisema mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika, Jean Ping.


"Habari kuhusu njama ya mapinduzi ni dhana tuu" alihakikisha kwa upande wake katibu mtendaji wa jumuia ya nchi zinazozungumza kireno,Domingos Simoes Pereira.


Na muakilishi wa katibu mkuu wa Umoja wa mataifa nchini Guinea Bissau, Joseph Mutaboba amesema:


"Sote tumepigwa na bumbuwazi.Mauwaji ya viongozi hawa wawili ni kisa cha kushutusha.Tunalaani vikali mauwaji haya."


Msemaji mkuu wa jeshi, José Zamora Induta, amekanusha ripoti kuhusu njama za mapinduzi na kusema "rais Bieira ameuliwa na kundi la watu ambao wao hawawajui.


Viongozi wa vikosi vya wanajeshi wamehakikisha jeshi litaheshimu katiba na demokrasia.


Kundi la wakuu wa vikosi vya wanajeshi limekutana na serikali ya waziri mkuu Carlos Gomes Junior.


"Katiba inaheshimiwa na kipindi cha mpito kinaongozwa hivi sasa na spika wa bunge, Raimundo Pereira" amesema katibu wa dola katika wizara ya mambo ya nchi za nje ya Ureno, Joao Gomes Cravinho.


Kwa mujibu wa katiba, spika wa bunge ndie anaestahiki kuongoza kipindi cha mpito na kuitisha uchaguzi mnamo muda wa siku 60 zitakazofuatia.


Serikali imetangaza siku saba za maombolezi na kumtaka mwanasheria mkuu aunde kamisheni kuchunguza mauwaji hayo.


Baraza la Amani na usalama la Umoja wa Afrika linakutana kwa dharura hii leo .Na jumuiya ya nchi zinazozungumza kireno ilikutana jana usiku mjini Lisbon na kutuma ujumbe mjini Bissau.Ujumbe mwengine unaotazamiwa kuwasili hii leo katika mji mkuu huo wa Guinee Bissau ni ule wa mawaziri wa jumuia ya ushirikiano wa kiuchumi wa nchi za Afrika magharibi-Ecowas.