1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pendekezo jipya la Waziri Mkuu wa Uingereza Magazetini

Oumilkheir Hamidou
22 Mei 2019

Uwezekano wa kuitishwa kura ya pili ya maoni kuhusu Brexit na miaka 70 ya sheria msingi ya Ujerumani ni miongoni mwa mada zilizochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani .

https://p.dw.com/p/3Iryo
England Brexit Rede Premierministerin Theresa May
Picha: Reuters/K. Wigglesworth

Tunaanzia Uingereza ambako waziri mkuu Theresa May amepania kwa kila hali kuyanusuru makubaliano yaliyofikiwa ya kuitoa nchi yake katika Umoja wa Ulaya-Brexit. Baada ya pendekezo lake kushindwa mara tatu bungeni, waziri mkuu May anakuja na pendekezo la nne na anakwenda umbali wa kuzungumzia uwezekano wa kuitishwa kura ya pili ya maoni ikilazimika. Gazeti la Badische Neueste Nachrichten linaandika: "Uwezekano wa kuitishwa kura ya pili ya maoni kuhusu mustakbali wa Uingereza katika Umoja wa Ulaya ni zawadi ya shingo upande kwa wafuasi wakakamavu miongoni mwa Tories na chama cha upinzani cha Labour. Ahadi alizotoa Theresa May hazitodumu muda mrefu, zitadumu hadi pale kiongozi mpya  wa wahafidhina na pengine mkakamavu zaidi, anaepinga Umoja wa Ulaya atakapochaguliwa na kulibatilisha pendekezo hilo.

Zaidi ya hayo wabunge hawana msimamo mmoja linapohusika na suala kama ni busara kuwauliza wananchi kwa mara nyengine tena suala lile lile ambalo tayari mwaka 2016 lilisifiwa rasmi  na kutajwa kuwa "Uamuzi wa kizazi kizima."Kuhusiana na pendekezo la Theresa May kuhusu uwanachama wa muda wa Uingereza katika Umoja wa forodha, wafuasi wa Labour hawatoona kama linakwenda mbali vya kutosha wakati ambapo pendekezo hilo halitokosa kuwapandisha hasira wafuasi wa chama cha kihafidhina-Tories pia. Kwa hivyo mtu anaweza kujiuliza yako wapi matumaini ya waziri mkuu ya kufanikiwa kuvunja upinzani bungeni?"

Wajerumani wanaadhimisha miaka 70 ya sheria msingi.

 Gazeti la mjini Cologne,Kölner Stadt Anzeiger linaandika:"Hakuna kinachodhihirika kuwa madhubuti zaidi humu nchini kama sheria hii yenye vifungu 146. Inajulikana wazi kabisa kuwa hiyo sio katiba-kwakuwa baada ya vita vikuu vya pili vya dunia sio wajerumani wote waliopata fursa ya kuchangia. Sheria msingi hii hata hivyo imeleta mizani katika nafsi, na utulivu katika shirikisho la jamahuri ya Ujerumani. Mpaka leo.

 Kwa upande mwengine , katika sheria msingi hiyo inayotumika tangu miaka 70 iliyopita yanadhaminiwa masuala muhimu ya kimaadili mfano haki sawa kati ya Mwanamme na Mwanamke, haki ya  juamii au  haki ya kumiliki. Kuna mengi ambayo hayajakamilika katika nukta hiyo. Na itatokea siku ambapo wajerumani hawatoweza tena kuepuka kuzusha mjadala kuhusu katiba.

.

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/ Inlandspresse

Mhariri: Sekione Kitojo