1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pendekezo la rais ni sumu

26 Januari 2014

Polisi imepambana na waandamanaji waliolizingira jengo moja mjini Kiev Jumapili(26.01.2014) wakati serikali ya Ukraine ikiwa mashakani baada ya Rais Viktor Yanukovych kukubali kuwapa viongozi wa upinzani nyadhifa za juu.

https://p.dw.com/p/1AxTg
Vitali Klitschko kiongozi mwenza wa upinzani akuhutubia mjini Kiev. (25.01.2014).
Vitali Klitschko kiongozi mwenza wa upinzani akihutubia mjini Kiev. (25.01.2014).Picha: picture-alliance/dpa

Mmojawapo wa mahasimu wakuu wa rais amelielezea pendekezo hilo kuwa ni jaribio la sumu la kuuwa vuguvugu la upinzani katika nchi iliotumbukia kwenye machafuko baada ya rais kugomea makubaliano ya ushirikiano na Umoja wa Ulaya na badala yake kuegemea makubaliano na upande wa Urusi.

Viongozi wa upinzani wanaoonekana kuzidi kupata ujasiri wamesema watashinikiza kuridhiwa zaidi kwa matakwa yao na hawatomuachia Yanukovych afanye atakavyo jambo ambalo linafanya kikao maalum cha bunge kilichopangwa kufanyika Jumanne ijayo kuwa mapambano makali ya kisiasa.

Katika vurugu mpya maelfu ya waandamanaji walijaribu kukivamia kituo cha utamaduni ambapo mamia ya askari wa usalama walikuwa wamekusanyika katikati ya Kiev mita chache kutoka kitovu cha maandamano ya wiki kadhaa dhidi ya serikali katika Uwanja wa Uhuru.

Waandamanaji walirusha mawe na mabomu ya moshi wakati polisi ikijibu kwa kufyetuwa maguruneti ya mshtuko na kuwarovya maji waandamanaji. Baadae polisi na wana usalama waliondoka kwenye jengo hilo kwa kupita katikati ya ujia uliowekwa na mlolongo wa watu baada ya kiongozi wa upinzani Vitalis Klitschko kuwasili katika eneo hilo na kusaidia kupata ufumbuzi wa makabiliano hayo. Makabiliano hayo ya saa mbili kabla ya alfajiri yamekuja baada ya Yanukovych kukubali kutowa ridhaa kubwa kabisa kwa mvutano huo wa miezi miwili ilioitumbukiza Ukraine kwenye mgogoro na kusababisha kuuwawa kwa watu watatu na kuzidisha mvutano kati ya Urusi na mataifa ya magharibi.

Waandamanaji wakijaribu kuvamia kituo cha utamaduni Kiev.(26.01.2014).
Waandamanaji wakijaribu kuvamia kituo cha utamaduni Kiev.(26.01.2014).Picha: picture-alliance/dpa

Kisa cha mzozo

Yanukovych ghafla alitelekeza mipango ya kusaini makubaliano ya ushirikiano wa kisiasa na biashara huru na Umoja wa Ulaya na badala yake kuahidi kuboresha uhusiano wake na Urusi mtawala wake wa zamani chini ya Muungano wa Kisovieti jambo ambalo limewaghadhabisha mamliloni ya watu wa nchi hiyo wenye ndoto ya kuwemo kwenye Umoja wa Ulaya. Akitaraji kukomesha maandamano hayo yenye kutishia kuizuwiya nchi hiyo ishindwe kuendesha shughuli zake Yanukovych hapo Jumamosi alikubali kumpa waziri wa zamani wa uchumi Arseny Yatsenyuk wadhifa wa waziri mkuu.

Rais Viktor Yanukovych wa Ukraine.
Rais Viktor Yanukovych wa Ukraine.Picha: picture-alliance/dpa

Klitschko bingwa wa zamani wa ndondi wa kimataifa amependekezwa kupatiwa wadhifa wa naibu waziri mkuu atakayeshughukilia masuala ya kibinaadamu. Ofisi ya rais imehusisha pendekezo lake hilo kwa masharti kwamba upinzani udhibiti maandamano hayo ya ghasia. Juu ya kwamba vugugugu hilo la maandamano kwa kiasi kikubwa ni la amani kundi la wale misimamo mikali limekuwa likiendesha mapambano dhidi ya polisi mbali na Uwanja wa Uhuru.

Uchaguzi na mapema

Viongozi wa upinzani ambao ngome yao iko miongoni mwa waandamanaji waliokusanyika katika uwanja wa uhuru ambao ulipewa jina baada ya Ukraine kujipatia uhuru wake kufuatia kusambaratika kwa uliokuwa Muungano wa Kisovieti hapo mwaka 1991 wamesema wataendelea kushinikiza uchaguzi wa mapema na kubatilishwa kwa sheria dhidi ya maandamano.

Waandamanaji wanaopinga serikali katika mji mkuu wa Kiev.(26.01.2014).
Waandamanaji wanaopinga serikali katika mji mkuu wa Kiev.(26.01.2014).Picha: picture-alliance/dpa

Yatsenyuk amekaririwa akiuambia umma baada ya mkutano wake na rais kwamba wako tayari kubeba jukumu la kuielekeza Ukraine kwenye Umoja wa Ulaya na kwamba jambo hilo litahusu pia kuachiliwa huru kwa waziri mkuu wa zamani Yulia Tymoshenko aliefungwa hapo mwaka 2011.

Klitschko ameliambia gazeti la Jumapili la Ujerumani la Bild am Sonntag " Hili ni pendekezo la sumu lililotolewa na Yanukovych kuligawa vuguvugu lao la maandamano dhidi ya serikali.Tutaendelea kuzungumza na kuendelea kudai uchaguzi wa mapema.Maandamano ya Waukraine dhidi ya rais mla rushwa hayapaswi kuwa hayana maana."

Viongozi wa upinzani wanasema Yanukovych ameisaliti Ukraine na wanatowa wito wa kufanyika kwa uchaguzi na mapema kabla ya ule uliopangwa kufanyika kipindi cha majira ya machipuko mwaka 2015. Klitschko anasema lazima ufanyike mwaka huu.

Ujerumani yahimiza kukomeshwa ghasia

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani hapo Jumapili amewataka Waukraine kujiepusha na matumizi ya nguvu na kutafuta suluhisho la kisiasa kwa mzozo wao unaopamba moto.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier.Picha: DW/B. Riegert

Frank-Walter Steimeier amesema taswira za kila siku zinazoonyeshwa kwenye televisheni kutoka Kiev na maeneo mengine ya nchi hiyo zinaonyesha kwamba hali sio tu ya wasi wasi bali ni mbaya hasa. Ameendelea kusema katika taarifa "Siku zijazo zinaweza kuamuwa njia itakayofuata mustakbali wa Ukraine."

Ameonya kwamba njia ya kuelekea Ukraine kwenye mustakbali wake itakaojiamulia yenyewe kwa hakika sio ile ya matumizi ya nguvu bila ya kujali inatokea upande gani. Amesema "Nina imani kwamba hata kama hali ni ngumu kiasi hiki,suluhisho la kisiasa bado ni jambo linalowezekana na lazima litafutwe."Kwa mujibu wa waziri huyo Ujerumani inawasiliana na serikali ya Ukraine,upinzani na washirika wenzao wengine wa Umoja wa Ulaya.

Marekani imemuonya Yanukovych kwamba kushindwa kuutuliza mzozo huo kunaweza kuathiri uhusiano wake na nchi hiyo.Urusi hapo Jumamosi imezidi kutowa onyo dhidi ya kuingiliwa kati kimataifa kwa mambo ya ndani ya Ukraine ukiiambia Umoja wa Ulaya izuwiye uingiliaje kati kutoka nje na kuihadharisha Marekani juu ya kutowa taarifa za kushadidia.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP

Mhariri: Sudi Mnette