1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pigo kubwa kwa wanariadha wa Urusi

17 Juni 2016

Shirikisho la Kimataifa la Riadha – IAAF limeamua kuitekeleza mafuruku yake dhidi ya wanariadha wa Urusi kutokana na matumizi ya dawa za kuongeza misuili nguvu

https://p.dw.com/p/1J8zI
China Peking olympisches Anti-Doping Labor
Picha: picture-alliance/dpa/G. Breloer

Hatua hiyo imeyaacha matumaini ya nchi hiyo kushiriki katika Michezo ya Olimpiki mjini Rio mikononi mwa wakuu wa Olimpiki kutoa uamuzi wao wiki ijayo.

IAAF ilikutana mjini Vienna jana kuamua kama ingeondoa marufuku hiyo baada ya kufahamishwa katika ripoti ya jopokazi kuwa matatizo makubwa ya matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni bado yanashuhudiwa Urusi. Marufuku hiyo ilitangazwa mara ya kwanza mwezi Novemba na kisha ikarefushwa mwezi Machi.

Kabla ya tangazo hilo la IAAF, Rais wa Urusi Vladmir Putin alisema wanariadha safi hawapaswi kuadhibiwa pamoja na wanaonaswa katika uovu huo. "Adhabu ya suala hili inapaswa kumlenga mtu binafsi. Haiwezi kuwashirikisha wote. Hauwezi kuwaadhibu wanamichezo wote kutoka shirikisho moja. Kama watu Fulani walikamatwa wakijihusisha na uovu huu, basi timu nzima haiwezi kuwajibishwa kwa vitendo vya mtu mmoja mwenye hatia. Nadhani hiyo ndo haki

Russland Wirtschaftsforum SPIEF 2016 in St. Petersburg
Rais Putin anasema wanariadha safi wasiadhibiwePicha: picture-alliance/dpa/Tass/M. Metzel

Uamuzi huo wa Urusi hata hivyo uligubikwa na habari za vyombo vya habari zilizodai kuwa rais wa IAAF Sebastian Coe alichukua hatua kwa kuchelewa sana kuhusiana na kashfa ya Urusi ya matumizi ya dawa za kuongeza misuli nguvu.

Pamoja na hayo, shirika la habari la BBC lilitoa ujumbe wa simu uliodokeza kuwa mtoto wa kiume wa mtangulizi wa Coe, Msenegal Lamine Diack, Papa Massata Diack, alipanga kura zilizompa ushindi Coe kuwa rais wa IAAF mwezi Agosti. Madai hayo yamekanushwa na IAAF. Tuhuma hizi zinaweza kuathiri juhudi za IAAF kupambana na mgogoro wake wa sasa kwa mujibu wa mkuu wa shirikisho la riadha la Ujerumani Clemens Prokop.

Na wakati Urusi imepata pigo kuhusiana na uamuzi wa IAAF, ni habari nzuri kwa Kenya, baada ya Shirika la Kimataifa la Kupambana na Matumizi ya Dawa zilizopigwa marufuku michezoni – WADA kuidhinidha sheria ya kudhibiti uovu huo katika mchezo wa riadha nchini Kenya. Waziri wa michezo Hassan Wario amesema kwenye Twitter kuwa WADA imeidhinisha sheria hiyo bila kuongeza tamko lolote, na sasa hatua inayofuata ni kutiwa saini na rais Uhuru Kenyatta.

Wario amesema hatua ya WADA sasa inawapa wanariadha wa Kenya nafasi ya kujiandaa bila hofu yoyote kwa Michezo ya Olimpiki inayoanza mwezi Agosti mjini Rio

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Khelef