1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Platini ajiondoa katika urais wa FIFA

8 Januari 2016

Rais wa UEFA aliyesimamishwa kazi Michel Platini ameendelea kujitetea kuwa hana hatia, licha ya kujiondoa katika katika kinyang'anyiro cha kuwania urais wa Shirikisho la Kandanda Duniani - FIFA

https://p.dw.com/p/1HaNO
Michel Platini
Picha: Getty Images/P. Schmidli

Platini anasema ataendelea kupambana ili kuibatilisha marufuku aliyopigwa ya miaka nane na kamati ya maadili ya FIFA mwezi jana, lakini sasa muda wa mwisho wa uchaguzi wa Februari 26 ni mfupi mno hali inayofanya nafasi yake ya kugombea kuwa ngumu.

Jaribio la Platini kumrithi Blatter na kuchukua wadhifa mkuu wa FIFA lilisimamishwa kwa sababu ya malipo aliyopokea kutoka kwa msiri wake huyo wa zamani mwaka wa 2011

Blatter na Platini walipigwa marufuku kwa miaka nane mwezi uliopita kutokana na hali ya mgongano wa maslahi katika malipo ya kiasi cha pauni milioni 1.35 ambayo pia yanafanyiwa uchunguzi wa kihalifu nchini Uswisi. Platini alilipwa Februari 2011, kabla ya Blater kuanza kampeni za kutaka kuchaguliwa tena dhidi ya Mohammed bin Hammam wa Qatar. UEFA iliyosimamiwa na Platini iliwataka wanachama wake wiki kadhaa kabla ya uchaguzi wa Juni 2011 kumuunga mkono Blatter, ambaye alichaguliwa bila kupingwa wakati Bin Hammam alituhumiwa kwa madai ya hongo.

Ni maafisa wachache wa FIFA waliofahamu kuhusu malipo ya Platini, ambayo yalifichuka wakati wa uchunguzi mpana wa Uswisi kuhusu masuala ya shirikisho hilo, ikiwa ni pamoja na tuhuma za ubadilishanaji wa fedha haramu wakati wa kutolewa vibali vya uwenyeji wa Kombe la dunia 2018 na 2022

Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Iddi Sessanga