1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Poland yapinga Tusk achaguliwe tena rais wa EU

9 Machi 2017

Poland imetishia kuchelewesha mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya utakaozungumzia mustakabali wa umoja huo, iwapo viongozi watamchagua kwa mara nyengine Donald Tusk kama rais, licha ya pingamizi kutoka kwa taifa hilo.

https://p.dw.com/p/2YuLm
Polen Donald Tusk
Rais wa EU Donald TuskPicha: picture alliance/dpa/A. Vitvitsky/Sputnik

Juhudi za serikali ya mrengo wa kulia ya Poland kumuondoa kwenye uongozi wa EU Tusk, aliyekuwa hasimu wao wa kisiasa nyumbani, zinatishia kuzua mgawanyiko wa magharibi na mashariki katika umoja huo, wakati unapojaribu kuweka fahamu katika umoja wake, wanapotazamia kusherehekea mwaka wa 60 tangu kubuniwa kwa EU.

Maafisa nchini Poland wanasema waziri mkuu Beata Szydlo anaweza kuyakataa yaliyoafikiwa katika mkutano huo, hivyo kufutilia mbali kuchaguliwa kwa Tusk aliyewahi kuwa waziri mkuu wa kitambo wa Poland au anaweza kusisitiza kuwepo kwa kura ya pamoja. Lakini wanadiplomasia wa Ulaya wanasisitiza kwamba Poland haina haki ya kukataa na kwamba waziri mkuu huyo wa kitambo, anaweza kuchaguliwa kwa wingi tu, kwani hawataki kubabaishwa na mzozo wa kinyumbani baina ya Tusk na serikali ya Poland.

Poland imempendekeza mbunge katika bunge la Ulaya Jacek Saryusz-Wolski achukuwe nafasi ya Tusk.

Merkel aunga mkono kuchaguliwa tena kwa Tusk

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametoa jawabu la haraka kuhusiana na juhudi hizo za kuzuia kuchaguliwa tena kwa Tusk, akisema ana uungwaji mkono mkubwa na kumpa muhula mwengine itakuwa ni ishara nzuri.

"Leo tutaamua kuchaguliwa kwa mara nyengine Donald Tusk kama rais wa Baraza la Ulaya kwa miaka mingine miwili unusu," alisema Merkel, "Naona kuchaguliwa kwake kama ishara ya mshikamano wa Umoja wote wa Ulaya. Nitafurahia kuendelea kushirikiana naye," aliongeza Kansela huyo.

Deutschland Merkel Regierungserklärung vor dem EU Gipfel
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani anamuunga mkono TuskPicha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Mzozo huo ambao ndio gumzo kubwa Alhamis, unayafanya kutoonekana na umuhimu mazungumzo kuhusiana na uchumi, ulinzi na hali ya wasiwasi iliyoko katika eneo la Balkan.

Mbali na hilo suala la Tusk, kumeebuka mgawanyiko pia kuhusiana na ule mpango wa azimio la Umoja wa Ulaya la mwongo mmoja ujao, litakalotolewa huko Roma, Italia, iwapo azimio hilo lijumuishe ule mpango uitwao "Ulaya inayokuwa kwa kasi."

Mataifa ya mashariki lakini yanahofia kwamba, mpango huo huenda ukaleta mfumo wa ubaguzi ambapo wanawachwa nyuma kwenye masuala kama ya sarafu ya yuro, uchumi na ulinzi, huku nchi zenye ushawishi mkubwa kama Ujerumani, Ufaransa, Italia na Uhispania zikisonga mbele.

Mwandishi: Jacob Safari/AFP/Reuters

Mhariri/Mohammed Abdul-Rahman