1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Poland yatekwa, Urusi yapepea

9 Juni 2012

Kinyang'anyiro cha UEFA EURO 2012 kiling'oa nanga huku kukishuhudiwa matukio chungu nzima katika mecho zote mbili zilizosakatwa. Katika mechi za kundi A, Poland ilitekwa nayo Urusi ikang'ara.

https://p.dw.com/p/15B9I
Source News Feed: EMEA Picture Service ,Germany Picture Service Referee Carlos Velasco Carballo of Spain (2nd L) shows a red card to Poland's goalkeeper Wojciech Szczesny (2nd R) during their Group A Euro 2012 soccer match against Greece at the National stadium in Warsaw, June 8, 2012. REUTERS/Pawel Ulatowski (POLAND - Tags: SPORT SOCCER)
Fussball Polen Griechenland Warschau UEFA EURO 2012Picha: Reuters

Timu inayopigiwa upatu katika kundi A Urusi iliiangamiza Jamhuri ya Czech magoli manne kwa moja, nayo Ugiriki ikaharibu karamu ya wenyeji wa dimba hilo Poland kwa kulazimisha sare ya goli moja kwa moja wakati timu zote mbili zikimaliza mchuano na wachezaji kumi kila upande.

Nahodha wa Urusi Andrei Arshavin alionyesha mchezo mzuri wakati timu yake ikionyesha umahiri wa mbinu ya mashambulizi mjini Wroklaw, Poland, na kuizika timu ya Czech.

Warusi sasa watacheza na Poland ambao walikuwa na mwanzo mzuri dhidi ya mabingwa wa UEFA EURO 2004 Ugiriki wakati mshambuliaji wao Robert Lewandoski alipotikisa wavu mapema lakini Wagiriki walijizatiti na hata wakashindwa kufunga penalti katika mchuano huo wa kusisimua.

Kuanza kwa mechi uwanjani kulisaidia kuondoa hofu dhidi ya tatizo la ubaguzi wa rangi katika kinyang'anyiro hicho, ambacho Poland inaandaa kwa pamoja na Ukraine na ndicho kikubwa zaidi cha aina yake mashariki mwa Ulaya tangu kuanguka kwa utawala wa kikomunisti.

Kipa Przemyslaw Tyton alikuwa chonjo na kuokoa penalti
Kipa Przemyslaw Tyton alikuwa chonjo na kuokoa penaltiPicha: Reuters

Mambo yangekuwa mabaya zaidi kwa timu ya nyumbani lakini kipa aliyeingia kama nguvu mpya Przemyslaw Tyton aliokoa penalti zikiwa zimesalia dakika 20 mchuano kukamilika.

Mlinda lango nambari moja wa Poland Wojciech Szczesny alionyeshwa kadi nyekundu baada ya kumtendea madhambi Dimitris Salpingidis katika eneo la hatari lakini mkwaju hafifu wake nahodha wa Ugiriki Giorgos Karagounis ukapanguliwa na Tyton.

Urusi yaiduwaza Jamhuri ya Czech

Katika mchuano wa pili Urusi ilifungua ukurasa wa magoli mawili ya kwanza yaliyofungwa na Alan Dzagoyev baada ya dakika 15 naye Roman Shirokov akaona wavu katika dakika ya 24 kabla ya Vaclav Pilar kuwafungia goli moja Waczech katika kipindi cha pili.

Dzagoyev aliongeza lake la pili katika dakika ya 79 naye nguvu mpya Roman Pavyluchenko akasukuma wavuni kombora zikiwa zimesalia dakika nane mechi kukamilika.

Poland na Ukraine wanataraji kuwa dimba hilo litauonyesha ulimwengu mafanikio yaliyopatikana tangu ukuta wa Berlin ulipoangushwa mnamo mwaka wa 1989 na Muungano wa Usovieti kuvunjika miaka miwili baadaye, huku Ukraine ikitaka fainali hizo ziisaidie kutangamana na mataifa ya magharibi.

Mlinda lango wa Czech Peter Cech alikuwa na kibarua kikali
Mlinda lango wa Czech Peter Cech alikuwa na kibarua kikaliPicha: Reuters

Hata hivyo nchi hizo mbili zinakumbwa na mgogoro kuhusu ubaguzi wa rangi, huku nchikadhaa zikipanga kususia dimba hilo kutokana na namna Ukraine inavyomnyanyasa kiongozi wa upinzani aliye gerezani Yulia Tymoshenko, katika kesi ambayo nchi za magharibi zinasema ilichochewa kisiasa.

Mechi zitakazochezwa nchini Ukraine zitaanza leo Jumamosi wakati Uholanzi itakapocheza na Denmark nayo Ujerumani kugaragazana na Ureno katika kundi gumu la B.

Kocha wa kikosi cha Ujerumani Joachim Löw huenda yuko tayari kukichagua kikosi chake kwa kuzingatia wachezaji kadhaa wa Bayern munich ambao walishindwa na Borussia Dortmund katika taji la Bundesliga kabla ya kushindwa na Chelsea kwa penalti katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Wachezaji hao ni kama vile Thomas Müller, Mario Gomez, Philip Lahm , Jerome Boateng, Manuel Neuer na Bastian Schweinsteiger…

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Sekione Kitojo