1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi Berlin yamkamata mshukiwa wa ugaidi

Sylvia Mwehozi
3 Novemba 2016

Raia mmoja wa Syria amekamatwa na polisi mjini Berlin, akishukiwa kuwa mwanachama wa taasisi ya kigeni ya kigaidi na anadhaniwa kwamba alikuwa na mipango ya kufanya mashambulizi katika mojawapo ya viwanja vya ndege.

https://p.dw.com/p/2S4Y3
Deutschland Syrer unter Terrorismus-Verdacht in Berlin festgenommen
Picha: picture-alliance/dpa/P. Zinken

Raia mmoja wa Syria amekamatwa na polisi mjini Berlin, Ujerumani akishukiwa kuwa mwanachama wa taasisi ya kigeni ya kigaidi na anadhaniwa kwamba alikuwa na mipango ya kufanya mashambulizi katika mojawapo ya viwanja vya ndege vya mji huo. Polisi wanaamini mshukiwa huyo ni mkimbizi wa kutoka Syria na amekuwa akiishi hapa nchini Ujerumani tangu mwaka jana. Kijana huyo aliye na miaka 27 anashukiwa na maafisa wa usalama kuwa mwanachama wa kundi linalojiita Dola la Kiislamu IS. Mshukiwa huyo alikamatwa katika nyumba katika wilaya ya Schoeneberg na uchunguzi tayari umekwisha anza. Mwendesha mashitaka wa serikali ambaye anashughulikia kesi nyingi za ugaidi hakumtaja jina mshukiwa huyo lakini akasema huenda kijana huyo ni mwanachama wa IS. Mwezi Oktoba maafisa wa usalama walimkamata mshukiwa mwingine aliyedhaniwa kuwa mkimbizi wa kutoka Syria kwa kupanga mashambulizi ya mabomu.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/jbh/kl (Reuters, dpa, AP)

Mhariri: Grace Kabogo