1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi Frankfurt na tuhuma za siasa kali za Mrengo wa kulia

Oumilkheir Hamidou
17 Desemba 2018

Polisi katika mji wa Frankfurt katika jimbo la Hesse inatuhumiwa kuhusika na siasa kali za mrengo wa kulia. Uchunguzi uliofanywa kufuatia vitisho dhidi ya wakili mmoja umethibtiisha hali hiyo.

https://p.dw.com/p/3AEew
Polizei Hessen
Picha: picture-alliance/dpa/S.Stein

 Gazeti mashuhuri la Ujerumabni Frankfurter Allgemeine limeandika katika toleo lake la Jumapili kwamba idara ya upelelezi ya jimbo la Hesse inachunguza tuhuma za kuwepo mtandao wa wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia miongoni mwa polisi wa jijini Frankfurt.

Idara ya upelelezi ya jimbo la Hesse imeunda tume maalum ya uchunguzi kufuatia madai kwamba baadhi ya maafisa wamemtumia barua ya vitisho wakili mmoja mwenye asili ya Uturuki aliyekuwa akiwawakilisha wafuasi wa itikadi kali ya dini ya Kiislam mahakamani.

Katika barua hiyo wakili huyo, Seda Basay-Yildiz ameitwa "nguruwe mchafu wa kituruki" na kutahadharishwa dhidi ya kutaka kuichafua Ujerumani."Bora utokomee haraka iwezekanavyo ikiwa unataka kuondoka salama, nguruwe we"-ndivyo ilivyoandikwa katika barua hiyo.

Wakili Seda Basay Yildiz
Wakili Seda Basay YildizPicha: DW/F. Hofmann

Vitisho vilivyokithiri dhidi ya mtoto wa miaka miwili

Basay Yildiz ameliambia gazeti la Frankfurter Neue Presse jumamosi iliyopita kwamba barua hiyo imepindukia barua za vitisho anazopokea, na kwamba ameingiwa na wasi wasi mkubwa zaidi kwasababu wanatishia kumdhuru binti yake mwenye umri wa miaka miwili.

"Tutalipiza kisasi.....tutamchinja binti yako" wameandika na jina la binti huyo kumtajka na pia mahala anakoishi. Barua hiyo imetiwa saini na kundi linalojiita "NSU2.0" likimaanisha kundi la chini kwa chini la siasa kali za mrengo wa kulia linalojiita "Wazalendo wa chini kwa chini wa kijamaa "-NSU , lililohusika na visa vya kigaidi mwisho mwa mjiaka ya 90 na kuwauwa wahamiaji wanane wenye asili ya Uturuki.. Basay-Yildiz amewatetea pia wahanga wa mashambulio ya NSU mahakamani.

Gari la polisi
Gari la polisiPicha: picture-alliance/dpa/M. Kusch

 Watuhumiwa watano wazuwiliwa kazi

Uchunguzi umeanza dhidi ya askari polisi watano , wanaume wanne na mwanamke mmoja, wanaotuhumiwa kubuni kundi hilo la asiasa kali za mrengo wa kulia katika polisi ya mjini Frankfurt. Wamesimamishwa kazi tangu kisa hicho kilipofichuliwa mapema mwezi wa Agosti uliopita.

Kwa mujibu wa gazeti hilo mashuhuri la Ujerumani baada ya kupokea barua hiyo wakili Basay-Yildiz aliwaarifu polisi ambao kwa upande wao wamegundua kuna wenzao wenye uwezo wa kupata maelezo ya watu binafsi kupitia komputa ya kituo cha polisi cha Frankfurt. Baada ya simu za mkononi na komputa zao kukamatwa katika nyumba za watuhumiwa hao ndipo wachunguzi wa polisi walipogundua ukweli wa mambno kuhusiana na kundi hilo la siasa kali za mrenmgo wa kulia.

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dw/AFP

Mhariri: Iddi Ssessanga