1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi inawashikilia zaidi ya watu 400 kufuatia ghasia mjini London

9 Agosti 2011

Polisi nchini Uingereza imewakamata watu watatu kutokana na jaribio la kutaka kumuuwa afisa mmoja wa polisi kwa kumgonga na gari usiku wa kuamkila leo. Hatua hiyo inafanya zaidi ya watu zaidi ya 400 kuwa mbaroni.

https://p.dw.com/p/12DOb
Polisi akiwa katika doriaPicha: dapd

Afisa mmoja wa kike wa polisi amefikishwa hospitali baada ya kugongwa na gari mjini Brent, huko kaskazini mwa London mapema asubuhi ya leo ingawa hali yake imeelezwa kuendelea vizuri. Mwanamke mwingine katika tukio hilo la ajali alipata majeraha madogo madogo.

Inaaminiwa kwamba ajali hiyo ilitokea wakati ambapo polisi waliamua kuingia barabarani kwa ajili ya kusimamisha baadhi ya magari yanayohisiwa kuwa na watu waliofanya uporaji katika duka moja la vifaa vya umeme.

Krawalle in Tottenham London
Vijana wakiwarushia mawe polisiPicha: AP

Vurugu hizo za siku tatu katika mji wa London na baadaye kuzagaa katika miji mingine mikubwa ya Uingereza zimetajwa kuyatia hasara ya mamilioni ya pauni makampuni ya bima.

Msemaji wa chama cha makampuni ya bima nchini Uingereza (ABI), Nick Starling amesema, kwa sasa ni mapema kuwa na taswira halisi ya hasara iliyotokea na hasa kuvurugwa kwa biashara, lakini makampuni hayo yanashughulikia uhalifu huo na yatatoa taarifa ya kina kutokana na hasara iliyopatikana.

Sehemu kubwa ya mji wa London imeathiriwa na vurugu hizo za siku tatu, zilizoambatana na vitendo vya uporaji vilivyofanywa na vijana waliovamia katika mitaa yenye maduka.

Ghasia hizi pia zimeathiri sekta ya michezo kimataifa, ambapo chama cha mpira nchini humo kimekatisha mchuano wa kimataifa kati ya Uingereza na Uholanzi uliopaswa kufanyika kesho.

Hali hakika ni mbaya, Waziri Mkuu wa Uingereza David Comeroon anatarajiwa kufanya mkutano wa dharura kujadili na baadaye kuzungumza na umma kupita vyombo vya habari.

Muonekano wa mji wa London umekuwa sio maridhawa ambapo hivi sasa mamlaka zinazohusika na usafi zinakabiliwa na changamoto kubwa ya kuusafisha mjini huo uliotapakaa mabaki ya chupa zilizovunjika, vioo pamoja na vipande vya matofali.

Wanasiasa na Polisi nchini humo wanasema ghasia hizo ni mbaya kuwahi kutokea katika miongo kadhaa.

Lakini wachambuzi pamoja na wakazi katika maeneo yalioathirika zaidi wanasema hali hiyo imetokana na ugumu wa maisha na hasa kutokana na tofauti kati ya walionacho na wasionacho.

Shirika la Habari la Uingereza-Reuters limemnukuu kijana mmoja akisema" Hatuna kazi, hakuna pesa. Tunasikia watu wengine wanapata vitu bure, kwa nini isiwe sisi" alihoji kijana huyo.

Profesa Gus Jonh wa chuo kikuu cha London alisema "Mkazo zaidi unatakiwa kuelekezwa kwa vijana wenyewe, lazima kuwepo na uwekezaji unaozingatia muda kwa vijana hao, kutokana kwa watu waliopata mafunzo katika jamii husika, wenye uwezo wa kufanya hivyo, kuhakikisha mabadiliko yanatokea miongoni mwa vijana wenyewe"

Kwa upande wao jeshi la Polisi linasema mpaka sasa limewatia kizuizini watu 334 mjini London, kiasi ya wengine 100 Birmingham. Ghasia zimezuka pia huko Bristol kusini/mashariki na kaskazini/mashariki mwa Liverpool.

Mwandishi: Sudi Mnette/RTR/DPA
Mhariri:Josephat Charo