1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi Kenya yawasaka walioshambulia mkutano Mombasa

5 Oktoba 2012

Polisi nchini Kenya hivi sasa ipo katika msako mkali kufuatia tukio la mauaji ya watu wanne na wengine kadhaa kujeruhiwa kwenye mashambulizi yaliyofanywa na watu wasiofahamika katika mkutano wa kisiasa mjini Mombasa.

https://p.dw.com/p/16L16
Wauguzi wakimuhudumia majeruhi wa ghasia za Tana River.
Wauguzi wakimuhudumia majeruhi wa ghasia za Tana River.Picha: Reuters

Mkutano huo ulitarajiwa kuhutubiwa na waziri ustawi wa uvuvi wa nchi hiyo, Amason Kingi,  ambaye alinusurika. Hii ni mara ya pili kwa mashambulizi kama hayo kufanyika ndani ya wiki moja katika eneo hilo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Agrey Adoli, ameiambia DW kwamba majeruhi wamepelekwa hospitali na wanaendelea vizuri. Kamanda Adoli amesema kwamba polisi haikuwa na taarifa kuhusu kufanyika kwa mkutano huo, na ndio sababu washambuliaji waliweza kuuvamia na kufanya mashambulizi hayo.

Miongoni mwa waliojeruhiwa ni aliyekuwa Jaji wa Mahakama ya rufaa nchini Kenya Stewart Madazayo ambaye ametangaza kuwania kiti cha useneta wa jimbo la Kilifi, kwenye uchaguzi mkuu Ujao hapo mwakani.

Namna mashambulizi yalivyofanyika

Mashambulizi hayo yalitokea wakati viongozi hao wa siasa walipofika katika uwanja wa shule ya Mtumondoni iliyoko Mtwapa nje kidogo tu ya Mji wa Mombasa, wakati  kundi la vijana wenye mapanga walipokwenda moja moja hadi kwenye jukwaa wakitaka kuukatiza mkutano huo.

Kijiji cha Chamwanamuma kikiwa kimechomwa kabisa kwa washambuliaji.
Kijiji cha Chamwanamuma kikiwa kimechomwa kabisa kwa washambuliaji.Picha: dapd

Mlinzi wa Waziri Kingi alikuwa wa kwanza kushambuliwa alipojaribu kutoa bastola yake, na kupata majeraha mengine ya panga kichwani. Hata hivyo, mlinzi huyo alifariki dunia muda mfupi tu baada ya kufika hospitalini.

Mgombeaji wa kiti cha useneta katika jimbo la Kilifi, Jaji Madzayo, ambaye ndio alikuwa jukwaani kuhutubia umati, alikatwa kwa panga kichwani na kuzimia na anaendelea kupata matibabu hospitalini.

Hata hivyo, umati uliokusanyika kuwasikiliza viongozi hao waliwazingira washambuliaji hao na kuwaua watatu miongoni  mwao. Mkuu wa Polisi wa wilaya ya Kilifi, Climent Wangai, anasema kuwa bado hakuna mshukiwa aliyekamatwa au kundi lolote kudai kuhusika na mashambulizi hayo.

Makundi ya FEDERESA na MRC yatajwa tena

Mashambulizi hayo yanatokea siku nne tu baada ya mashambulizi mengine kama hayo kufanyika katika eneo la Ganze ambako watu 15 waliuawa baada ya kundi la majambazi wanaodaiwa walikuwa wakila kiapo kwa lengo la kutekeleza mashambulizi kuuawa na wanakijiji.

Mapigano katika mtaa wa mabanda wa Mathare nchini Kenya mwaka 2008.
Mapigano katika mtaa wa mabanda wa Mathare nchini Kenya mwaka 2008.Picha: picture-alliance/dpa

Wakati wa mkasa huo, polisi walidai kukamata bendera ya kundi  linalojiita FEDERESA, ambalo linadai kuwa limeunda serikali yake iliyo na baraza la mawaziri 17.

Kundi la Mombasa Republican Council (MRC) ambalo ni vuguvugu linalopigania ukombozi wa mkoa wa Pwani, na ambalo linanyooshewa kidole kuhusika na mashambulizi ya aina hii, limepinga vikali kuhusika na visa hivi huku likiishtumu serikali "kwa njama  ya kutaka kulitia lawamani", kwa mujibu wa msemaji wa kundi hilo, Mohammed Mraja.

Katika siku za hivi punde visa vya mashambulizi yanayofanywa na watu wasiojulikana vinaongezeka katika eneo la mkoa wa Pwani, kwa kiwango cha kutia hofu.

Mwandishi: Eric Ponda/DW Mombasa
Mhariri: Mohammed Khelef