1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Macedonia yazidiwa na wakimbizi

Isaac Gamba21 Agosti 2015

Polisi wa Macedonia wamewatawanya wakimbizi waliokwama mpakani na Ugiriki ikiwa ni siku moja tu baada ya kutangaza hali ya hatari ya kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi wanaoelekea Ulaya.

https://p.dw.com/p/1GJd7
Polisi wakikabiliana na wakikmbizi kwenye mpaka wa Macedonia na Ugiriki.
Polisi wakikabiliana na wakikmbizi kwenye mpaka wa Macedonia na Ugiriki.Picha: picture-alliance/dpa/G. Licovski

Kundi la wahamiaji wapatao 3,000 ambao walitumia muda wa usiku kucha katika eneo la wazi mpakani walifanya majaribio kadhaa ya mashambulizi hii leo kupambana na polisi wa Macedonia baada ya mpaka kufungwa hapo jana ili wasiweze kuvuka.

Takribani watu wanane walijeruhiwa katika tukio hilo ikiwa ni pamoja na kijana mmoja ambaye alionekana kuvuja damu kutokana na kujeruhiwa na guruneti ambalo lilirushwa katika msongamano wa watu.

Askari polisi wakiwa na magari yaliyobeba silaha walisambaza nyaya zenye meno ya ncha kali katika njia za reli zinazotumiwa na wahamiaji kuvuka kutokea ugiriki kwenda Macedonia.

Ugiriki imekumbana na wimbi la wahamiaji mwaka huu ambalo halijawahi kutokea wengi wao wakikimbia vita na migogoro nchini Syria na Afghanistan wakivuka mara nyingine kwa kificho kuingia katika visiwa vyake wakitokea maeneo ya pwani ya karibu ya Uturuki ambapo zaidi ya wakimbizi 160,000 wamewasili hadi sasa.

Wimbi ni kubwa

Wimbi kubwa hili la wakimbizi limeistua serikali ya Ugiriki hususani katika visiwa vyake ambavyo vingi vyake vina maeneo madogo kwa ajili ya watalii wanaofika kutembelea na havina uwezo wa kuhudumia idadi kubwa ya wakimbizi wanao wasili.

Polisi wakikabiliana na wakikmbizi kwenye mpaka wa Macedonia na Ugiriki.
Polisi wakikabiliana na wakikmbizi kwenye mpaka wa Macedonia na Ugiriki.Picha: Reuters/A. Avramidis

Ni wachache tu kati ya wahamiaji wanaowasili wanataka kubakia Ugriki, taifa ambalo kwa sasa linakabiliwa na hali mbaya ya kiuchumi. Wengi wao huelekea moja kwa moja katika maeneo ya kaskazini kwenye mpaka wa nchi hiyo na Macedonia wanakodandia treni zinazokwenda kasikazini kupitia Serbia na Hungary, lengo likiwa kufika katika mataifa ya Ulaya yaliyostawi zaidi kiuchumi, yakiwemo Ujerumani, Uholanzi na yale ya Scandinavia.

Mmoja wa wakimbizi katika eneo hilo la mpakani alisikika akisema ya kuwa kuna idadi kubwa ya wakimbizi ambao bado wako njiani kuja kwa ajili ya kuvuka kupitia mpaka huo.

"Kuna watu zaidi ya 3000 bado wanaendelea kuja huwezi kuamini kinachotokea hapa mpakani hivi sasa kwani wanajua fika kuwa hatutakaa hapa na wala hatuna mpango wa kuchukua kazi zao," alisema mkimbizi huyo.

Msemaji wa jeshi la polisi la Macedonia Ivo Kotevsik alisema polisi na jeshi watadhibiti eneo la kilomita 50 mpakani ili kudhibiti wimbi la wakimbizi wanaotaka kuingia nchini humio kutokea Ugiriki, akiongeza kuwa hatua hiyo ni maalumu kwa ajili ya usalama wa raia wa nchi hiyo waishio mpakani.

Mwandishi: Isaac Gamba/APE/EAP
Mhariri: Iddi Ssessanga