1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi nchini Israel wasema Netanyahu ashtakiwe

Zainab Aziz
14 Februari 2018

Polisi nchini Israel wanataka waziri mkuu Benjamin Netanyahu ashtakiwe lakini mwanasheria wake amesema mapendekezo ya polisi kuhusu mashtaka ya rushwa dhidi ya waziri mkuu huyo hayana msingi.

https://p.dw.com/p/2sgir
Israel Benjamin Netanyahu
Picha: picture-alliance/AP Photo/R. Zvulun

Polisi nchini Israel imesema Waziri mkuu wa nchi hiyo Benjamin Netanyahu anapaswa kushtakiwa kuhusu tuhuma za rushwa zinazomkabili. Taarifa iliyotolewa na polisi imesema, kuwa wana ushahidi wa kutosha wa kuweza kumtia hatiani waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa makosa yanayohusiana na ufisadi pamoja na kuvunja uaminifu hizo zikiwa ni kesi mbili tofauti. Hali hiyo imesababisha  aibu na pigo kubwa kwa waziri mkuu huyo na pia inaweza kuchochea miito ya kumtaka ajiuzulu.

Kufuatia tamko hilo la polisi la tangu jana Jumanne, Netanyahu kwa hasira amekanusha tuhuma zote zinazomkabili ambazo zinajumuisha kupokea karibu dola 300,000 kama zawadi kutoka kwa mabilionea wawili.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu
Waziri mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Reuters/N. Elias

Bwana Netanyahu amewashutumu polisi kuwa wanamwandama lakini ameapa kuendelea kubakia madarakani na amesema atagombea wadhfa wake kwenye uchaguzi mpya. Uchaguzi wa bunge nchini humo umepangwa kufanyika Novemba mwakani. 

Mapendekezo hayo ya polisi dhidi ya waziri mkuu Benjamin Netanyahu yamefikisha mwisho wa uchunguzi uliokuwa unafanyika kwa zaidi ya mwaka mmoja juu ya madai kwamba Netanyahu alikubali zawadi kutoka kwa kigogo wa Hollywood Arnon Milchan na bilionea wa Australia James Packer, na vilevile tuhuma kwamba aliahidi kutoa upendeleo kwa gazeti la nchi hiyo la Yediot Aharonot ili liweze kuyadhibiti magazeti shindani, ilimradi gazeti hilo lichapishe taarifa nzuri tu za waziri mkuu huyo.

Mapendekezo hayo ya polisi sasa yatapelekwa kwa Mwanasheria Mkuu Avihai Mendelblit, ambaye atachunguza ushahidi kabla ya kuamua iwapo atamfungulia mashtaka bwana Netanyahu.  Netanyahu anaweza kuendelea kuhudumu katika wadhfa wake wakati wa uchunguzi huo, unaotarajiwa kuendelea kwa miezi kadhaa.

Waziri mkuu wa zamani wa Israel Ehud Barak
Waziri mkuu wa zamani wa Israel Ehud BarakPicha: picture-alliance/dpa/Tv_Grab

Hata hivyo wapinzani nchini Israel, wamemtaka Netanyahu ajiuzulu kutokana na tuhuma hizo dhidi yake. Waziri Mkuu wa zamani Ehud Barak, mpinzani mkuu wa Netanyahu, alimemtaka ajiondoe mwenyewe kutoka madrakani na vyama vinavyounda serikali vimteue kiongozi mwingine haraka.

Hata hivyo waziri wa Fedha Moshe Kahlon, mwanachama muhimu, katika muungano huo wa vyama vinavyoungda serikali iliyopo madarakani amesema Netanyahu hatajiuzulu isipokuwa mwanasheria mkuu wa Israeli atoe agizo rasmi la kuondolewa Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.

Mwandishi: Zainab Aziz/APE/DPAE

Mhariri: Iddi Ssessanga