1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi watibua maandamano ya kupinga mizigo kupitia SGR

Faiz Musa,DW,Mombasa7 Oktoba 2019

Nchini Kenya maafisa wa polisi katika mji wa bandari wa Mombasa wameyatibua maandamano ya kupinga agizo la mizigo  bandarini Mombasa kubebwa kwa reli ya kisasa SGR kuelekea Nairobi

https://p.dw.com/p/3QpNQ
Miglieder Fast Action Movement Nyali Police Station
Picha: DW/F. Musa Abdallah

Viongozi wa maandamano hayo na watetezi wa haki za binadamu ni miongoni mwa waliokamtwa.Watu kumi na tatu wamekamatwa katika maandamno hayo yaliyokuwa yamekaribia katika daraja la Nyali kutoka eneo la Kengeleni - Kongowea  Kazkazini mwa mji Mombasa. Katibu mtendaji wa vuguvugu la wafanyabiashara la Fast Action lilokuwa likiongoza maandamano hayo Harriet Mugenda ni miongoni mwa waliokamatwa.

Mwenyekiti wa vuguvugu hilo Salim Karama amesema serikali imewafanyia maovu wafanyabishara hao wanaotetea haki zao kwa njia za kisheria baada ya  kupewa kibali cha kufanya maandamano hayo.

Waandamaji hao wamekamatwa kwa madai kwamba maandamno yao yalikuwa yanafunga shughuli za usafiri katika barabara ya kipekee ya daraja la Nyali inayounganisha kisiwa cha Mombasa na eneo bunge la Nyali na Kisauni ambapo asubuhi huwa na shughuli nyingi za watu kuingia mjini Mombasa.

Mmoja wa waandamaji hao Margaret Ambasa ameilaumu idara ya serikali kwa kutumia nguvu dhidi ya wenzao licha ya maandamno hayo kuwa ya Amani.

Waliokamatwa kufikishwa mahakamani

Idara ya polisi inatarajiwa kuwafikisha mahakamani waandamanaji hao waliokamatwa wakiwa na viongozi kutoka shirika la haki za bindamu la Muhuri na Haki Afrika na kuwafungulia mashtaka ya kufanya maandamano ya fujo.

Salim Karama Fast Action Movement
Mwenyekiti wa vuguvugu la wafanyabiashara la Fast Action Salim Karama Picha: DW/F. Musa Abdallah

Mbunge wa Mvita aliye pia mwenyekiti wa kamati ya uwekezaji katika bunge la kitaifa Abdulswamad Nassir ndiye kiongozi wa kipekee wa kisiasa aliyehudhuria maandamano.

Waziri wa uchukuzi James Macharia wiki jana alirudia kusema kwamba amri ya mizigo kusafirishwa kwa reli ya kisasa ya SGR imesimamishwa kwa muda kwa ajili ya mazungumzo lakini wafanyabiashara hao wanaeleza kwamba agizo hilo linaendelea kufanyakazi na tayari kulingana na ripoti watu zaidi ya elfu mbili waliokuwa wameajiriwa na kampuni za kibinafsi za malori ya kubeba mizigo hiyo wamefutwa kazi.