1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi yataka Netanyahu ashitakiwe kwa madai ya ufisadi

Caro Robi
2 Desemba 2018

Polisi wa Israel wamesema wamapata ushahidi wa kutosha wa mashitaka ya rushwa na udanganyifu wa fedha kufunguliwa dhidi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na mke wake.

https://p.dw.com/p/39Ht1
Israelischer Premier Benjamin Netanjahu
Picha: AFP/Getty Images/J. Hollander

Inadaiwa kwamba Netanyahu na kampuni ya Bezeq telecom walifanya makubaliano yanye thamani ya mamilioni ya dola ili shirika la habari la Walla ambalo ni kampuni ndogo ya Bezeq liwe linachukua mtazamo chanya wakati linaporipoti taarifa zinazomhusu Netanyahu.

Netanyahu amekanusha madai dhidi yake. Iwapo atafunguliwa mashitaka, waziri huyo mkuu wa Israel anayetumikia muhula wa nne madarakani atakabiliwa na mojawapo ya changamoto kubwa zaidi kisiasa.

Uamuzi wa mwisho wa iwapo Netanyahu atafunguliwa mashitaka au la utachukuliwa na mwanasheria mkuu wa Israel ambaye bado anatafakari iwapo amshitaki kuiongozi huyo na kesi nyingine mbili zinazomkabili za madai ya hapo awali ya rushwa, udanganyifu na uvunjaji wa uaminifu.

Mwanasheria mkuu kutoa maamuzi

Madai hayo yanahusiana na Netanyahu kukubali zawadi kutoka kwa wafanyabiashara na kujaribu kufikia makubaliano ya kibiashara na wamiliki wa vyombo vya habari kumuangazia kwa njia bora zaidi na badala yake kuyabana magazeti yanayoonekana washindani wa wafanyabiashara aliongia mkubaliano nao.

Argentinien Buenos Aires Benjamin Netanjahu  AMIA Zentrum
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na mke wake SarahPicha: picture-alliance/AP /Israeli Government

Wengi wa washirika wa Netanyahu katika serikali ya mseto wamesema watasubiri maamuzi ya mwanasheria mkuu kabla ya kuchukua hatua yoyote kuhusu madai yanayomkabili.

Wachambuzi kadhaa wasema huenda Netanyahu akaitisha uchaguzi wa mapema iwapo mashitaka yatafunguliwa dhidi yake. Uchaguzi ujao Israel unatarajiwa mwezi Novemba 2019, lakini huenda kiongozi huyo wa Israel akawania tena na hivyo kumlazimu mwendesha mashitaka mkuu kutafakari upya kabla ya kumfungulia mashitaka.

Polisi pia imesema imepata ushahidi wa kutosha kumfungulia mashitaka ya rushwa Shaul Elovitch, rafiki wa karibu wa familia ya Netanyahu. Elovitch alikuwa mwenyekiti wa kampuni ya Bezek na mwanahisa mkubwa wa kampuni hiyo. Mwingine ambaye polisi wanataka afunguliwe mashitaka ni aliyekuwa mkurugenzi mkuu mtendaji wa kampuni hiyo Stella Handler.

Elovitch na Handler wamekanusha madai dhidi yao. Walikamatwa na kuzuiwa kwa muda mapema mwaka huu na wameshajiuzulu kutoka kampuni hiyo ya Bezeq.

Muda mfupi baada ya polisi kutoa mapendekezo yao ya kufunguliwa mashitaka dhidi ya Netanyahu, mke wake na washirika wake, Netanyahu ametoa taarifa kusema madai dhidi yake hayana msingi wowote kisheria na mwishowe hakutakuw na lolote litakalotokana na uchunguzi dhidi yake kwani hakuna lolote.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/Afp

Mhariri: Yusra Buwayhid