1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi yawakamata waandamanaji Hong Kong wanaopinga China

Bruce Amani
1 Oktoba 2020

Dazeni kadhaa za waandamanaji wanaounga mkono demokrasia wamekamatwa kisiwani Hong Kong Alhamisi kwa kukiuka marufuku ya kufanya maandamano wakati mji huo ukiadhimisha siku ya kitaifa ya China

https://p.dw.com/p/3jIJ0
Hongkong Demonstranten werden verhaftet
Picha: Tyrone Siu/Reuters

Jamhuri ya Watu wa China inaadhimisha Oktoba mosi kuasisiwa kwake kwa kuandaa matamasha mbalimbali. Lakini kisiwani Hong Kong, imekuwa siku ya huzuni kwa wale wenye wasiwasi kuhusu hatua ya serikali ya kimabavu ya China kuendelea kuwakandamiza wapinzani.

Kiongozi wa Hong Kong Carrie Lam na maafisa waandamizi wa China bara walihudhuria sherehe iliyofanyika chini ya ulinzi mkali wa polisi na vizuizi vya usalama.

"Katika miezi michache iliyopita, ukweli usiopingika mbele ya kila mmoja ni kuwa amani imerejea katika jamii yetu” Lam alisema katika hotuba yake.

"Usalama wa kitaifa wa nchi yetu umelindwa mjini Hong Kong na raia wetu wanaweza tena kutekeleza haki zao na uhuru kwa mujibu wa sheria.”

Hongkong 71. Nationalfeiertag der Volksrepublik China
Maadhimisho ya Siku ya Kitaifa ya ChinaPicha: Lam Yik/Reuters

Masaa kadhaa baadaye polisi wa kupambana na ghasia waliwavamia watu waliokuwa wakiandamana na kupaza sauti katika eneo moja maarufu la kibiashara mjini humo.

Polisi imesema karibu watu 60 wakematwa, wengi wao kwa kosa la kukusanyika kinyume cha sheria.

Siku ya taifa ya mwaka jana, maadhimisho ya miaka 70 ya Jamhuri ya Watu wa China ilizusha makabiliano makali kati ya waandamanaji na polisi wakati wa maandamano ya miezi saba ya kudai demokrasia ambayo yaliigubika Hong Kong.

Mamlaka zilikataa kutoa kibali cha maandamano ya mwaka huu, zikitaja hofu ya usalama na marufuku ya mikusanyiko ya zaidi ya watu wanne kutokana na janga la virusi vya corona.

Kwa zaidi ya miezi 16, zaidi ya watu 10,000 wamekamatwa wakati wa maandamano huku mahakama zikishuhudia mrundiko wa kesi, zikiwemo za viongozi wa maandamano.

afp, ap