1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Pompeo awasili Saudi Arabia kwa mazungumzo na washirika wake

Amina Mjahid Sekione Kitojo
24 Juni 2019

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo amewasili mjini Jeddah kwa mazungumzo na washirika wake wa Mashariki ya Kati, wakati kukiwa na mvutano kati ya Marekani na Iran

https://p.dw.com/p/3Kyx7
USA Außenminister Pompeo reist nach Saudi-Arabien
Picha: picture-alliance/dpa/J. Martin

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani atakayeendelea na safari yake hadi Umoja wa Falme za kiarabu, aliwaambia waandishi habari kabla ya kuondoka Marekani kuelekea Jeddah kwamba nchi yake ingelipenda kuwa na mazungumzo na Iran hata wakati inapopanga kuiekea nchi hiyo vikwazo vipya vya kiuchumi. 

Mike Pompeo amesema atazungumza na viongozi wa Saudi Arabia pamoja na Umoja wa Falme za kiarabu ili kuwa na mbinu za kujipanga na kuhakikisha wanaungana kuunda muungano wa kidunia dhidi ya Iran.

Mohammed bin Salman al-Saud ist der Kronprinz, Verteidigungsminister und stellvertretende Premierminister Saudi-Arabiens
Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed Bin SalmanPicha: picture-alliance

Uhusiano kati ya maadui wa muda mrefu Iran na Marekani, umezidi kudorora tangu rais Trump alipoiondoa Marekani mwaka mmoja uliopita kutoka katika makubaliano ya mwaka 2015 juu ya mpango wa nyuklia wa Iran, ambapo Iran ilitakiwa kusitisha shughuli zake za nyuklia ili ilegezewe vikwazo ilivyoekewa.

Mvutano umeendelea kupamba moto baada ya mashambulizi ya hivi karibuni ya matanki ya mafuta katika eneo la Guba, ambapo Marekani inailaumu Iran kuhusika na shambulizi hilo, kudunguliwa kwa ndege isiyokuwa na rubani ya Marekani wiki iliyopita na mashambulizi ya mara kwa mara katika viwanja vya ndege vya Saudia vimezidisha uadui uliopo kati ya nchi hizo mbili. 

Hata hivyo Iran imekanusha kuhusika na shambulizi la matanki katika eneo la Guba ambako hadi sasa hakuna kundi lolote au mtu yeyote aliyekiri kuhusika.

Uingereza ina wasiwasi wa kutokea vita vya kutokusudia kati ya Marekani na Iran

Kwa upande wake Uingereza kupitia Waziri wake wa mambo ya kigeni Jeremy Hunt imesema haidhani kama Marekani au Iran inataka kuanzisha vita lakini ina wasiwasi kuwa vita vya kutokusudia huenda vikatokea.

Hunt amesema kwa sasa wanafanya kila wawezalo ili kutuliza cheche za maneno kati ya nchi hizo mbili. Ameongeza kuwa nchi yake imekuwa na mawasiliano ya karibu na Marekani juu ya hali katika eneo la Guba.

Großbritannien London | Mike Pompeo, US-Außenminister & Jeremy Hunt, Außenminister
Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo na mwenzake wa Uingereza Jeremy Hunt Picha: Reuters/H. McKay

Huku hayo yakiarifiwa haijhawa wazi iwapo Waziri huyo wa mambo ya kigeni wa Marekani atajadili suala la mauaji ya mwandishi habari na mkosoaji mkubwa wa serikali ya Saudi Arabia Jamal Khashoggi, baada ya ripoti ya Umoja wa Mataifa wiki iliyopita kumtaka mwanamfalme Mohammed Bin Salman na maafisa wengine wa juu serikalini kuchunguzwa baada ya ushahidi wa kutosha kutolewa dhidi yao.

Utawala wa Rais Trump unaushinikiza ule wa Saudi Arabia kuwafikisha mbele ya sheria wale wote waliohusika na mauaji yaKhashoggi, na kuutaka ufanye hivyo kabla ya mwaka mmoja kutimia baada ya kuuwawa kwake Oktoba 2 katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul.

Vyanzo: Reuters/AFP