1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin akutana na Umoja wa Ulaya

Admin.WagnerD21 Desemba 2012

Rais wa Urusi Vladmir Putin anakutana na viongozi wa Umoja w Ulaya, katika mazungumzo ya kwanza kati ya rais huyo na umoja huo tangu kuchaguliwa kwake, ambayo yatagubikwa na Syria, biashara, na haki za binaadamu.

https://p.dw.com/p/177PD
Rais wa Urusi Vladimir Putin, rais wa halmashauri ya Ulaya, Jose Manuel Barroso na rais wa baraza la Ulaya Herman Van Rompuy.
Rais wa Urusi Vladimir Putin, rais wa halmashauri ya Ulaya, Jose Manuel Barroso na rais wa baraza la Ulaya Herman Van Rompuy.Picha: picture-alliance/dpa

Uhusiano kati ya kanda hiyo yenye wanachama 27 na Urusi, ambayo ndiyo mgavi wake mkuu wa nje wa nishati, na mshirika muhimu wa kibiashara, umekumbwa na mizozo juu ya mabomba ya kusafirisha gesi, na migogoro mingine kuhusu magari na nguruwe. Viongozi wa Ulaya wamekosoa vikali kufungwa jela kwa wanamuziki wa kundi la Pussy Riot, kukandamizwa kwa viongozi wa upinzani na sheria zinazozuia maandamano na mashirika yanayofadhiliwa kutoka nje tangu Putin alivyochaguliwa tena mwezi Mei mwaka huu.

Rais Putin (wa pili kushoto) wakati wa kuanza kwa mazungumzo kati ya nchi yake na Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Disemba 21, 2012.
Rais Putin (wa pili kushoto) wakati wa kuanza kwa mazungumzo kati ya nchi yake na Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Disemba 21, 2012.Picha: Reuters

Matarajio ni madogo sana

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton, alisema mwezi Septemba mwaka huu kuwa hatua hizo za Urusi zina mwelekeo unaotia wasiwasi mkubwa kwa Umoja wa Ulaya. Maafisa wa Urusi na wale wa Umoja wa Ulaya hawategemei kuwepo na ufanisi katika mazungumzo kati ya Putin na rais wa halmashauri ya Ulaya, Jose Manuel Barosso, na rais wa baraza la umoja huo, Herman Van Rompuy. Wadadisi wengine wameonyesha kushangazwa kwamba Putin anahangaika kufanya ziara hiyo ya mjini Brussels.

Mtaalamu wa masuala ya Urusi katika shirika la ushauri la Chatham House la jijini London, James Nixey, amesema mikutano michache iliyopita kati ya Urusi na Umoja wa Ulaya ilikuwa na ufanisi mdogo sana na kwamba anadhani rais Putin anafanya zoezi lisilo na manufaa sana. Hakutarajiwi kuwepo na makubaliano juu ya mgogoro wa Syria, ambako Urusi inatofautiana na msimamo wa mataifa ya magharibi juu ya mgogoro huo ambao umegharimu maisha ya watu zaidi ya 40,000 tangu kuanza kwa uasi dhidi ya rais Bashar al-Assad mwezi Machi mwaka 2011. Ufaransa na mataifa mengine ya magharibi wameikosoa Urusi kwa kuyapigia kura ya turufu, maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yaliyolenga kumshinikiza rais Assad.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton.
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton.Picha: AFP/Getty Images

Mgogoro wa nishati kati ya Urusi na Umoja wa Ulaya

Sula la nishati ambalo limekuwa chanzo cha mgogoro kati ya Brussels na Moscow linatarajiwa kuyagubika mazungumzo ya leo. Ulaya inaitegemea Urusi kwa karibu robo ya mahitaji yake ya gesi asilia, lakini katika muongo uliopita, utawala mjini Moscow umekuwa na mfulululizo wa misuguano na majirani zake wa muungano wa zamani wa Kisovieti - Ukraine na Belarus, ambao umevuruga usafirishaji wa gesi barani Ulaya. Migogoro hiyo iliulazimu Umoja wa Ulaya kubadilisha ugavi kutoka kwa Urusi.

Rais wa Ukraine alijiondoa katika mazungumzo ya ugavi wa gesi na Putin katika dakika za mwisho siku ya Jumanne, na kuongeza wasiwasi juu ya uhakika wa ugavi wa nishati hiyo kwa Umoja wa Ulaya. Halmashuri ya Umoja wa Ulaya iliongeza wasiwasi kati ya Ulaya na Moscow mwezi Septemba, baada ya kuanzisha uchunguzi kuhusiana na vitendo visivyo vya ushindani vinavyofanywa na kampuni kubwa ya nishatri la Urusi, Gazprom.

Ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi nchini Urusi.
Ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi nchini Urusi.Picha: dapd

Umoja wa Ulaya watishia kuipeleka Urusi WTO

Migogoro ya kibishara nayo inatarajiwa kuchukua nafasi kubwa katika mazungumzo ya mjini Brussels, ambayo yatawajumuisha pia waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi, Sergio Lavrov, waziri wa nishati Alexander Novak, na waziri wa uchumi Andrei Belousov. Kamishna wa biashara wa Umoja wa Ulaya, Karel De Gucht, alisema mwezi huu kuwa Urusi inachelewa kutatua migogoro ya kibishara na umoja huo kuhusu kila kitu kuanzia kwenye nguruwe hadi kwenye magari, na alitishia kuipeleka katika shirika la kimataifa la biashara, WTO.

Umoja wa Ulaya unasema Urusi, ambayo ilijiunga na WTO mwaka huu baada ya kusubiri kwa miaka 19, ilikuwa inayatoza kodi isivyo haki, magari kutoka umoja huo, na kuzuia bila sababu, usafirishaji wa wanayama hai kutoka umoja huo, na kufanya usafirishaji wa bidhaa mbalimbali za umoja huo kuwa wa gharama, hasa mbao.

Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/rtre
Mhariri: Josephat Nyiro Charo