1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Putin na Rouhani wazungumzia mpango wa Nyuklia

9 Januari 2014

Rais Vladimir Putin wa Urusi na mwenzake wa Iran, Hassan Rouhani, leo wamefanya mazungumzo juu ya makubaliano ya mpango wa nyuklia wa Iran.

https://p.dw.com/p/1Ao2C
Mazungumzo ya mpango wa Nyuklia yafanyika Geneva.
Mazungumzo ya mpango wa Nyuklia yafanyika Geneva.Picha: Atta Kenare/AFP/Getty Images

Kiongozi mkuu wa Iran, Ayatullah Ali Khamenei, ameikosoa Marekani kutokana na msimamo wake kuelekea nchi yake.

Ayatollah Ali Khamenei ameyaita mazungumzo ya mpango wa nyulkia wa nchi yake na viongozi wa mataifa yenye nguvu duniani kuwa yanaonesha wazi uadui wa jadi wa Marekani dhidi ya taifa lake na Waislamu wote.

"Tulishatangaza awali kwamba katika masuala mengine, tukiona ni lazima, tutazungungumza hata na shetani, ili kuondosha uovu wake," amesema Khamenei akitumia jina la shetani kumaamisha Marekani.

Kauli hiyo ya kiongozi huyo wa juu kabisa wa Iran, inakuja muda mfupi kabla ya kuanza rasmi kwa mazungumzo juu ya utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani juu ya udhubiti wa mpango huo wa nyuklia mjini Geneva, Uswisi.

Iran na Umoja wa Ulaya wanatarajia kuanza mazungumo ya kina kupanga mikakati ya utekelezaji wa makubaliano yao yaliyofikiwa mwezi Novemba, kudhibiti mpango wa nyuklia wa Iran.

Mazungumzo hayo yanahudhuriwa pia na naibu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, anayeshughulikia masuala ya siasa, Wendy Sherman.

Makubaliano hayo ya Geveva yaliandaliwa ili kusitisha mradi wa nyuklia wa Iran kwa kipindi cha miezi sita, huku pakitafutwa makubaliano ya mwisho na ya kudumu.

Rais wa Iran Hassan Rouhani aahidi kupunguza kiwango cha kutengwa nchi yake.
Rais wa Iran Hassan Rouhani aahidi kupunguza kiwango cha kutengwa nchi yake.Picha: Isna

Rouhani afanikisha azma ya kupunguza vikwazo

Fursa za diplomasia ziliongezeka baada ya Iran kumchagua Hassan Rouhani kuwa rais hapo mwezi Juni mwaka jana.

Kiongozi huyo ameahidi kupunguza kiwango cha kutengwa Iran na jumuiya ya kimataifa na akafanikiwa kupunguza vikwazo.

Ndani ya makubaliano hayo Iran italazimika kupunguza shughuli zake za kiatomiki, ambazo mataifa ya Magaharibi yanashuku kuwa zinaweza kutengeneza mabomu ya nyuklia.

Kwa upande wao, mataifa hayo yataondosha baadhi ya vikwazo ambavyo vimeliathiri taifa hilo ambalo uchumi wake unatagemea mafuta. Iran imekuwa ikisisitiza kwamba mpango wake wa nyuklia ni kwa ajili ya matumizi ya amani na si kivita.

Katika hatua nyengine, Rais Vladimir Putin wa Urusi, amezungumza kwa njia ya simu na mwenzake wa Iran, Hassan Rouhani, juu ya mkutano huo ya nyuklia wa Geneva na pia mazungumzo ya amani ya Syria.

Kwa mujibu wa taarifa ya ikulu ya Urusi, Kremlin, viongozi hao wawili walijadiliana masuala kadhaa ya kimataifa, ikiwemo matayarisho ya mkutano wa pili wa Geneva, juu ya amani ya Syria.

Iran italazimika kupunguza shughuli za kiatomiki.
Iran italazimika kupunguza shughuli za kiatomiki.Picha: AP

Hadi sasa, haijawa wazi kuwa Iran itakuwa miongoni mwa watakaohudhuria mkutano huo wa amani wa Syria utakaofanyika wiki ijayo na kuhudhuriwa na mataifa 30 nchini Uswisi.

Mwandishi: Flora Nzema/AFP/RTRE

Mhariri: Mohamed Khelef