1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia 10, muasi wa ADF wauwa katika mapigano Beni

Iddi Ssessanga
29 Machi 2018

Raia 10 na muasi mmoja waliuawa katika mapigano kati ya jeshi la Congo na waasi katika mji wa Beni, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, ambako makundi ya waasi wanawania udhibiti wa utajiri wa rasilimali.

https://p.dw.com/p/2vCvS
Symbolbild Opfer der ADF
Picha: Getty Images/AFP/K. Mailro

Vurugu hizo zilitokea siku ya Jumanne jioni wakati waasi waliposhambulia ngome za jeshi karibu na mji wa Beni, katika mkoa wa Kivu kaskazini, alisema Kapteni Mak Hazukay wakati akizungumza na shirika la habari la Ufaransa AFP. "Tumeonrodhesha maiti za raia 10 mpaka sasa," alisema.

Muasi kutoka kundi la Allied Democratic Forces (ADF), aliuawa pia, alisema, na kuongeza kuwa mapigano yalikuwa yakiendelea. Michel Kakule, daktari mkuu katika hospitali ya Beni, aliliambisha shirika la AFP kuwa baadhi ya waathirika, "walikuwa na majeraha ya risasi wakati wengine walishambuliwa kwa mapanga."

Shambulio hilo lilizusha hasira miongoni mwa wenyeji, "waliozuwia barabara kadhaa kuu katika mji huo kupiga mauaji ya raia 10," alisema Gilbert Kambale, anaefanya kazi na shirika la kiraia.

Demorkatische Republik Kongo - Soldaten der Democratic Republic of Congo nach Kämpfen mit Rebellen
Wanajeshi wa jeshi la Kongo (FARD) wanaopigana dhidi ya ADF katika mkoa wa Kivu Kaskazini.Picha: Reuters/G. Tomsaevic

Tangu Januari, vikosi vya jeshi la Kongo vimeshiriki katika operesheni kubwa dhidi ya ADF lakini havijaweza kukomesha umuagaji damu ndani ya Beni na maeneo jirani.

"Kundi la ADF sasa linaendesha vita visopacha - tunapowashambulia katika eneo moja, wanajibu kwa kutushambulia kwingineko," alisema Hazukay. ADF ni moja ya makundi kadhaa ya silaha yanayoshikilia maeneo mashariki mwa DRC, ambayo yanapambana kudhibiti rasilimali za eneo hilo tajiri.

Kundi hilo la waasi, lilioundwa na Waislamu wenye itikadi kali waliokuwa wanapinga utawala wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni, limekuwepo Kivu Kaskazini tangu 1995 ambako linatuhumiwa kuuwa mamia ya raia katika kipindi cha miaka mitatu na nusu iliopita.

Limetuhumiwa pia kwa kuuwa wanajeshi 15 wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania, katika shambulio baya eneo la Beni Desemba mwaka uliopita.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/AFPE

Mhariri: Saumu Yusuf