1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Iran Shahram Amiri arejea nyumbani

Josephat Nyiro Charo15 Julai 2010

Amiri anadai alitekwa nyara na maajasusi wa Kimarekani mwaka mmoja uliopita, amewasili mjini Tehran na moja kwa moja kukanusha taarifa kwamba alikuwa mwanasayansi. Alihojiwa na maafisa wa Israel alipokuwa Marekani

https://p.dw.com/p/OM61
Shahram Amiri, kushoto, akiwa na babake mjini TehranPicha: AP

Shahram Amiri ambaye alitoweka alipokuwa anahudhuria Ibada ya Hajj nchini Saudia Arabia mwaka jana- alipewa mapokezi ya kishujaa alipowasili mapema leo asubuhi katika uwanja wa ndege wa Imam Khomeini, mjini Tehran.

Na mmoja kwa mmoja akafichua kuwa yeye si mwanasayansi na mtaalamu wa nyuklia bali ni mtafiti wa kawaida tu ambaye anayefanya kazi katika chuo kikuu mjini Tehran.

Akizungumzia masaibu yake- Amiri alisema aliteswa kisaikologia na kiafya- na kwamba yeye kutekwa nyara ilikuwa ni njama ya Marekani kuwakera kisaikologia Iran na kutoa taarifa za kupotosha dhidi ya utawala huo kiislamu.

Kulingana na mwanasayansi huyo- kulikuwepo na maafisa wa Israel mara kadhaa alipokuwa anahojiwa- na kwamba aliona ishara kuwa waliokuwa wanamzuiliwa walikuwa na mpango wa kumsafirisha nchini Israel.

Maafisa nchini Iran daima wameshikilia kuwa Amiri alitekwa nyara na wapelelezi wa Marekani CIA, vyombo vya habari vya Marekani navyo vimedai kuwa Amiri alikuwa ameiasi Iran alipofika Marekani. Marekani imekanusha madai yote kwamba Amiri alikuwa anazuiliwa nchini humo.

Akizungumza katika mkutano huo wa waandishi wa habari Amiri alisema atafichua yote katika siku kadhaa zijaazo, kwa sababu hivi sasa kuna masuala ambayo ni nyeti na yanaweza kutishia usalama wa kitaifa. Pia alipuuzilia mbali madai ya Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton kwamba yeye Amiri alikuwa nchini Marekani kwa hiari na kwamba ana uhuru wa kuondoka nchini humo wakati wowote anaotaka.

Na bado kulikuwa na ufichuzi zaidi, pale mwanasayansi huyo aliposema CIA walitaka kumlipa dolaa milioni 50 ili aisaliti Iran pamoja na kutoa taarifa za ndani kuhusiana na mpango wa nyuklia wa Iran.

Kabla ya kuwasili mjini Tehran, katika mahojiano na televisheni ya kitaifa ya Iran, Amiri alisema alitekwa nyara na watu waliokuwa na bunduki alipokuwa njiani kuelekea katika msikiti katika mji wa Madina, Saudia Arabia. Aliwekwa ndani ya gari na baadaye alidungwa sindano ya usingizi na kusafirishwa kwa ndege ya kijeshi hadi nchini Marekani. Kumekuwepo na sintofahamu kuhusiana na sakata hii ya Amiri hasa baada ya kanda mbili za video kuibuka mwezi mmoja uliopita.

Ukanda wa kwanza ulimuonyesha Amiri akisema anazuiliwa na maajasusi wa Marekani na ukanda wa pili ulikuwa pia na uso wa Amiri akisema kwamba aliwasilia kwa hiari Marekani na anasoma katika chuo kimoja kikuu huko Arizona.

Mwandishi: Munira Muhammad/ AFPE

Mhariri: Josephat Charo