1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa nje wakimbia Sudan ya Kusini

Abdu Said Mtullya21 Desemba 2013

Raia wa nje wanayakimbia mapigano Sudan ya Kusini. Hadi sasa watu zaidi ya 500 wameshauawa, wakati Marekani inapeleka mjumbe.

https://p.dw.com/p/1AeQW
Wanajeshi wa serikali ya Sudan Kusini.
Wanajeshi wa serikali ya Sudan Kusini.Picha: Getty Images

Mapigano baina ya makabila yanayopingana yameendelea na kuenea nchini kote katika Sudan ya Kusini. Kwa mujibu wa taarifa, nchi kadhaa zinapeleka ndege ili kuwaondoa raia wao.

Wakati huo huo mawaziri wa nchi za Afrika wamemtaka Rais Salva Kiir aanze mazungumzo na aliekuwa Makamu wake, Riek Machar ili kuutaua mgogoro.

Lakini idadi ya vifo imeongezeka na Umoja wa Mataifa umelaani kuuliwa kwa askari wake wawili kutoka India katika shambulio lililofanywa kwenye kambi yake moja. Raia 11 pia waliuawa kutokana na shambulio hilo.

Raia waliokimbia mapigano wakisubiri nje ya ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Bor, jimboni Jonglei.
Raia waliokimbia mapigano wakisubiri nje ya ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Bor, jimboni Jonglei.Picha: picture-alliance/dpa

Umoja wa Mataifa umearifu kwamba vijana wapatao 3000 waliokuwa na silaha walikusanyika kwenye kambi nyingine katika sehemu ya Bor kwenye jimbo la Jonglei ambako raia 14,000 wamekimbilia ili kuyaepuka mapigano.

Kwa mujibu wa taarifa watu wasiopungua 500 wameuawa kutokana na mapigano baina ya watu wa kabila la Rais Kiir na watu wa kabila la Nuer la aliekuwa Makamu wake, Machar.

Umoja wa Mataiafa umesema watu zaidi ya 35,000 wamekilimbilia kwenye maeneo yake mbalimbali nchini kote. Habari zaidi zinasema kwamba uwanja wa ndege wa Juba umejaa raia wa nje wanaotaka kuondoka Sudan ya Kusini ili kuepuka vurumai.

Uingereza yapeleka ndege ya pili
Uingereza imepeleka ndege ya pili ya kijeshi ya uchukuzi ili kuwaondoa wananchi wake kutoka Sudan ya Kusini. Kampuni ya mafuta ya China pia imeanza hatua za kuwaondoa wafanyakazi wake kutoka nchini humo.

Marekani nayo imewaweka askari 45 ili kuzilinda mali zake na pia imeufunga ubalozi wake mjini Juba. Rais Obama ametahadharisha kwamba Sudan ya Kusini imesimama pabaya.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-Moon amezilaani ghasia zinazoendelea katika Sudan ya Kusini na ametoa mwito wa kufanya juhudi ili kurejesha amani nchini nchini humo.

Wakati huo huo majeshi ya Uganda yamewasili mjini Juba ili kuwaondoa raia wa Uganda walionaswa katika mapigano.

Waziri Kerry atuma mjumbe
Na habari kutoka Washington zinasema kuwa Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry anamtuma mjumbe maalumu wa Marekani wa masuala ya Sudan ya Kusini ili kusaidia katika juhudi za kuanzisha mazungumzo baina ya pande zinazopingana.

Waziri John Kerry.
Waziri John Kerry.Picha: Reuters

Kerry amesema huu ndio wakati kwa viongozi wa Sudan ya Kusini wa kuchukua hatua za kuyadhibiti makundi yao yenye silaha, ili kukomesha mashambulio dhidi ya raia na kuacha kufanya mashambulio ya kulipizana kisasi. Waziri Kerry aliyasema hayo wakati akiutangaza mpango wa kumtuma mjumbe wake maalumu wa masuala ya Sudan bwana Doland Booth.

Kerry ameeleza kuwa uamuzi wa kumpeleka mjumbe maalumu umefikiwa wakati ambapo mapigano yanaendelea nchini Sudan ya Kusini kote, baina ya makabila yanayopingana. Amesema uamuzi huo pia unatokana na mazungumzo ya simu baina yake na Rais Salva Kiir.

Waziri Kerry alimpigia simu Rais huyo wa Sudan ya Kusini hapo jana kumtaka achukue hatua za kuwalinda raia wote na kumtaka afanye juhudi za kuanzisha mazungumzo.

Mwandishi: Mtullya Abdu/apf,rtre
Mhariri: Ssessanga Iddi