1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wa Sudan Kusini wanalengwa katika mapigano yaliyozuka upya

22 Februari 2014

Umoja wa Mataifa umesema raia wa ndiyo walengwa wakuu wa ghasia zilizozuka upya nchini humo zilizosababisha vifo vya maelfu ya watu, wengine kubakwa, kukamatwa, kuteswa, mali kuporwa na nyumba zao kuchomwa moto.

https://p.dw.com/p/1BDgc
Picha: Reuters

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS) hapo jana ulitoa ripoti yao ya kwanza kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu katika mzozo huo wa Sudan Kusini kati ya tarehe 15 mwezi Desemba hadi tarehe 31 mwezi Januari.

Ripoti hiyo inatoa taswira ya ghasia zilizoibuka kutokana na mapigano makali kati ya wanajeshi wa Rais Salva Kiir ambaye anatokea kabila la Dinka na wapiganaji wa waasi wanaomtii aliyekuwa makamu wa rais wa nchi hiyo, Riek Machar, ambaye ni wa kabila la Nuer.

Ripoti hiyo iliyokusanya ushahidi kutoka kwa watu 500 wakiwemo walioshuhudia mapigano hayo, waathiriwa, maafisa wa serikali na wa usalama, imeonyesha kuwa raia wa nchi hiyo na wa kigeni walilengwa kimakusudi katika mauaji makubwa, kupotea kwa watu, kubakwa na kuteswa na wapiganaji wa pande zote mbili zinazozozana.

Kutokana na kuwa uchunguzi huo bado unaendelea kuhusiana na visa hivyo vya ukiukjai wa haki za binadamu, wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wamesema ni mapema kutathmini iwapo ghasia za kingono zilitumika kama silaha katika vita hivyo.

Raia wanalengwa kimakusudi

Ripoti hiyo ya awali inaangazia madai hayo ya ukiukaji wa haki za bindaamu katika majimbo manne ambayo yameathirika zaidi na mapigano hayo nayo ni Equatoria ya Kati, Jonglei, Unity na Upper Nile.

Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini Hilde Johnson
Mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa Sudan Kusini Hilde JohnsonPicha: Charles Atiki/AFP/Getty Images

Serikali inasisitiza kuwa ghasia hizo zilichochewa na jaribio lililotibuka la kuipindua serikali lililofanywa na wanajeshi watiifu kwa Machar. Makamu wa rais huyo wa zamani aliyefukuzwa kazi na Kiir anakanusha madai hayo ya kutaka kuipindua serikali, lakini amesema lengo lake ni kuona Kiir anaondolewa madarakani.

Huku kilichochea hasa mzozo huo kikiendelea kuwa kitendawili, ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa inasema mzozo huo umesababisha janga kubwa la kiusalama, ukiukaji wa haki za binadamu na kusababisha uhasama wa kikabila katika taifa hilo changa zaidi duniani.

Ukabila unazidisha uhasama

UNMISS imesema katika mapigano yaliyozuka upya katika mji wa Malakal, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Upper Nile kuna ushahidi wa kutosha kuwa raia wameuawa kimakusudi wakiwemo watoto wawili waliouawa nje ya kambi ya Umoja wa Mataifa.

Wanajeshi wa Sudan Kusini mjini Juba
Wanajeshi wa Sudan Kusini mjini JubaPicha: Charles Lomodong/AFP/Getty Images

Waasi wanashutumiwa kuhusika katika mauaji hayo ya raia katika mji wa Malakal waliolengwa kutokana na misingi ya kikabila. Hata hivyo, hata wanajeshi wa serikali SPLA pia wanashutumiwa kuwalenga raia wa kabila la Nuer hasa katika mji mkuu wa nchi hiyo Juba.

Ripoti hiyo pia inasema mahojiano na waathiriwa wa mzozo huo pia inadokeza kuwa wanawake, wengi wao raia wa kigeni kutoka Kenya, Uganda, Ethiopia na Eriteria walibakwa na magenge katika miji ya Rubkona na Bentiu kati ya tarehe 17 na 27 mwezi Desemba na wanaotuhumiwa kuwa waasi.

Mwandishi: Caro Robi/AP/AFP

Mhariri: Mohammed Khelef