1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Raia wakimbia mapigano

Martin, Prema4 Februari 2008

Hali ya utulivu yarudi kwa muda N'djamena waasi wakiapa kurudi tena kwa vita

https://p.dw.com/p/D26h
Wakimbizi wa Chad wakielekea CameroonPicha: picture-alliance/ dpa

Hali ya utulivu imerejea katika mji mkuu Ndjamena  baada ya siku mbili za mapigano makali baina ya waasi wanaotaka kuipindua serikali ya rais Idrss Deby na wanajeshi wa serikali.Kwa mujibu wa mwandishi habari wa kituo cha Reuters aliyeko katika mji huo hakuna milio ya risasi wala mapigano yanayoendelea kwa tangu alfajiri ya leo huuku maelfu ya watu wakichukua nafasi hiyo kuuhama mji wa NdjamenaKatika eneo la mto Longone Chari maelfu ya raia wa Chad wameonekana wakitoroka mapigano  kuelekea nchini Cameroon.Akizungumza  akiwa mjini Addis Ababa nchini Ethiopia waziri wa mambo ya nje wa Chad Amad Allam Mi ameiambia redio moja ya Ufaransa kwamba mapigano yamemalizika katika mji mkuu wa Ndjamena lakini ameshutumu vikali Sudan kwa kuuchochea moja kwa moja ghasia hizo za waasi.

Hata hivyo waasi wa Chad wanasema mapambano hajakwisha ila wamejiondoa kwa muda katika mji mkuu Ndajmena kwa ajili ya kuwapa nafasi raia waondoka katika eneo hilo.Kiongozi mmoja wa waasi aliyekataa kutaja jina akizungumza na shirika la habari la Afp ameonya kwamba watu wasifikiria rais Deby kashinda mapambano hayo.

Ijumaa iliyopita waasi walipambana vikali wanajeshi karibu na eneo la makaazi ya rais ambako rais Deby alikuwa amejificha,maiti zilionekana zimetapakaa kote katika barabara za mji mkuu huku mashirika ya kutoa msaada yakiwasaidia maelfu ya wengine waliokuwa wamejeruhiwa kufuatia mapigano hayo.

Rais wa Tanzania Jakaya mrisho Kikwete ambaye ni mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika akiizungumzia hali ya Chad akiwa mjini Addis Ababa Ethiopia aliowaonya waasi juu ya kutaka kuchukua kwa nguvu madaraka akisema Umoja huo utaitenga serikali yoyote itakayoingia kwa nguvu madarakani.


Waziri wa mambo ya nje wa Chad bwana Allam Mi amesema Sudan inahusika katika kupanga opresheni hizo za waasi kwa lengo la kutaka kuweka utawala wanaouunga mkono mjini N'damena na kuufunga mlango juu ya mzozo wa Darfur.

Aidha waziri huyo ametishia kuivamia Sudan kuwasaka waasi.

Kufuatia mapigano hayo makali mamia ya raia wakigeni wamekuwa wakiondolea nchini humo,wanajeshi wa Ufaransa  wanaweka usalama wa hali ya juu katika maeneo ambako raia wakigeni wamekusanyika kusubiri kusafirishwa kutoka nchini humo.Jeshi hilo la Ufaransa limesema tarayi limeshawasafirisha raia wakigeni 580 kutoka mjini mkuu Ndamena na kuwapeleka mjini Librevile nchini Gabon.baadhi ya  raia 320 wakigeni waliosalia wanatazamiwa kusafirishwa hii leo.Rais Sarkozy wa Ufaransa ameyalaani mapigano hayo ya Chad huku Baraza la usalama la Umoja wa mataifa likianza kikao kingine juu ya mgogoro huo wa Chad baada ya hapo jana kushindwa kutoa tamko la pamoja juu ya  vita hivyo.

Duru za jeshi la ufaransa zinasema kuna kiasi cha waaasi 2000 huku serikali ikiwa na wanajeshi kiasi cha 2000 hadi elfu 3000.waasi wakisaidiwa na helikopta za Sudan na ndege nyingine za kivita aina ya Antonov katika mapambano ya jana kwenye eneo la mji wa Andre mashariki mwa Chad karibu na mpaka na jimbo la Darfur nchini Sudan.Serikali ya Sudan lakini imekanusha madai hayo ikisema mapigano ya Chad ni suala la ndani ya Chad na wala haliwahusu.