1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ufaransa: Matokeo yatangazwe bila upendeleo

Mjahida31 Agosti 2016

Tume ya uchaguzi ya Gabon Cenap imempitisha Rais Ali Bongo kuwa mshindi wa uchaguzi kwa kujipatia asilimia 49.85 ya kura ikilinganishwa na mpinzani wake Jean Ping aliyepata kura 48.16 ya kura.

https://p.dw.com/p/1JtCo
Rais wa Gabon Ali Bongo
Rais wa Gabon Ali BongoPicha: Reuters/G.W.Obangome

Baada ya matokeo hayo kuwekwa wazi upande wa kiongozi wa upinzani Jean Ping, Ulitaka kura hizo kuhesabiwa tena katika mkoa wa Haut Ogooue, uliokuwa na idadi kubwa ya watu waliyojitokeza kupiga kura karibu asilimia 99.98 alisema msemaji wa Ping.

Hata hivyo matokeo rasmi yanatarajiwa kutangazwa rasmi na waziri wa mambo ya ndani katika hotuba yake kwa Taifa moja kwa moja kupitia televisheni ya kitaifa

Awali wakati Rais Bongo alipokuwa anasubiri matokeo, Chama tawala kilitoa wito wa kuwa na matokeo ya kuaminika ili kuendelea kudumisha amani. Chama hicho cha Gabonese Democratic Party) PDG kinaunga mkono nafasi ya mgombea wake Ali Bongo lakini kinalenga kudumisha amani, alisema Austin Boukoubi.

Aidha raia wengi wa nchi hiyo tajiri kwa mafuta wanahofu ya kutokea tena vurugu kama ilivyoshuhudiwa katika uchaguzi wa mwaka 2009. Hofu hii imetokea baada ya uchaguzi wa siku ya Jumamosi ambako Bongo na Ping wote walidai kushinda uchaguzi huo.

Rais Ali Bongo na mpinzani wake Jean Ping
Rais Ali Bongo na mpinzani wake Jean PingPicha: picture-alliance/dpa/E.Laurent/L.JinMan

Huku hayo yakiarifiwa wafuasi wa Ping wameanza kutoa malalamiko yao kuelekea matokeo hayo kutangazwa rasmi, huku waangalizi wa Umoja wa Ulaya waliyopigwa marufuku kuingia katika kikao cha tume ya uchaguzi wakisema uchaguzi huo haukuendeshwa kwa njia ya uwazi.

Umoja wa Ulaya wasema matokeo lazima yawekwe wazi

"Umoja wa Ulaya unarejelea tena wito uliyotolewa na mkuu wa ujumbe wa waangalizi kwamba matokeo ya kila kituo cha kupigia kura yanapaswa yawekwe wazi," alisema msemaji wa mkuu wa sera za kigeni wa Umoja huo Federica Mogherini katika taarifa yake. Kuanzia hapo jana tume hiyo imekuwa ikijadili matokeo yaliyo na utata katika moja ya mikoa tisa ya nchi hiyo katika eneo lililo na kundi la kikabila la rais Ali Bongo.

Chini ya watu 628,00 walisajiliwa kupiga kura katika nchi hiyo koloni la zamani la Ufaransa iliyo na idadi ya watu milioni 1.8. Kwengineko msemaji wa Wizara ya mambo ya nje wa Ufaransa amesema Gabon ni lazima ionyeshe uwazi na kutopendelea wakati matokeo rasmi yatakapochapishwa.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja huo Federica Mogherini
Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja huo Federica MogheriniPicha: Getty Images/AFP/P. Huguen

Rais Ali Bongo aliye na umri wa miaka 57 alichukua madaraka kwa mara ya kwanza baada ya Kifo cha Babake Omar Bongo, baadaye alishinda uchaguzi wa mwaka 2009 uliyokumbwa na ghasia za baada ya uchaguzi zilizosababisha kuchomwa ubalozi wa Ufaransa katika mji wa mafuta wa Port Gentil nchini humo.

Mwandishi Amina Abubakar/AFP/Reuters

Mhariri: Iddi Ssessanga