1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Bush atangaza mpango wa kuondoa wanajeshi 8000 Iraq

Saumu Mwasimba9 Septemba 2008

Wanajeshi zaidi wa Mareakani watapelekwa Afghanistan

https://p.dw.com/p/FEzr
Picha: AP

Rais wa Marekani George W Bush ametangaza mpango wa kuwaondoa wanajeshi kiasi cha 8,000 kutoka nchini Iraq kufikia mwezi wa Februari mwakani na badala yake kutuma wanajeshi zaidi nchini Afghanistan.

Rais Bush ameutaja mpango huo uliopendekewa na Generali Patreaus kuwa umetokana na kuimarika kwa hali ya ulasama nchini Iraq na kwamba kutafungua njia ya kupelekwa wanajeshi zaidi nchini Afghanistan katika miezi ya hivi karibuni.

Wanajeshi wa majini waliokuwa wapelekwe Iraq mwezi Novemba sasa watakwenda Afghanistan wakifuatiwa na kikosi cha wanajeshi wa nchi kavu.

Aidha rais Bush amesema wanajeshi 8000 wataondolewa kutoka nchini Iraq kufikia mwezi Februari ikiwa ni pamoja na wanajeshi 1000 kutoka mkoa wa Anbar watakaondolewa mwezi Novemba mwaka huu.Rais Bush aliongeza kusema kwamba

''Kupungua kwa kiwango cha ghasia nchini Iraq kumedumu kwa miezi mingi,tumepunguza kiwango cha mashambulio,wanajeshi wa Iraq wanaendelea kuwa na uwezo wa kuongoza na kushinda vita hivi,kutokana na hali hiyo tumepitisha sera ya kuwarudisha nyumbani wanajeshi kiasi fulani kama hatua ya mafanikio.Wakati hali ikiendelea kuimarika nchini humo tutavirudisha nyumani vikosi vyote vitano vya nchi kavu,majini na wale waliopelekwa Iraq kama sehemu ya kuongeza wanajeshi nchini humo.''

Uamuzi huo wa rais Bush huenda ukawa ndio wa mwisho katika vita vya Iraq.

Kwa sasa kuna wanajeshi laki moja na 46 elfu nchini Iraq na 33 elfu nchini Afghanistan.Maamuzi yoyote ya muda mrefu kuhusu hatua ya baaadae ya kutuma wanajeshi yatakuwa mikononi mwa atakayemrithi rais huyo wa Marekani mwezi wa Januari.

Hata hivyo idadi hiyo iliyotangazwa ni ndogo mno na pia mwendo wa kuondolewa wanajeshi hao sio kama ilivyotarajiwa kwa muda mrefu hali ambayo inaonyesha malengo ya wanajeshi na rais Bush ya kutotaka kuuhujumu usalama ulioanza kuimarika nchini Iraq.

Wakati hayo yakiarifiwa mjumbe wa zamani wa Umoja wa ulaya katika Afghanistan Francesc Vendrell ameushutumu utawala wa Bush kwa kujipotosha katika mwelekeo wake nchini Afghanistan.

Mjumbe huyo amesema sera ya Marekani kuelekea Afghanistan inabidi kuangaliwa upya lakini hilo haliwezi kufanyika ikiwa rasi Bush bado yuko madarakani.

Mwezi uliopita waziri mkuu wa Iraq Nouri al maliki alisema kwamba ingawa ratiba ya kuwaondoa wanajeshi watakaosalia Iraq haijapangwa amekubaliana kimsingi na jeshi la Marekani kuondoa wanajeshi wa kigeni kufikia mwaka wa 2011.

Kwa hivi sasa serikali ya Iraq inaendelea na mazungumzo kuhusu makubaliano ya kiusalama juu ya hatma ya wanajeshi wa Marekani nchini Iraq kabla ya kumalizika muda uliowekwa na Umoja wa mataifa.

►◄