1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Bush kuelekea Saudi Arabia

Josephat Charo14 Januari 2008

Rais atajaribu kutafuta kuungwa mkono katika mazungumzo ya amani baina ya Israel na Palestina

https://p.dw.com/p/CpKA
Rais George W Bush (kulia) akikaribishwa na Aida Abdullah Al- Azdi, mfanyakazi wa taasisi ya mafunzo na utafiti ya jumuiya ya nchi za kiarabu kabla kutoa hotuba yake katika hoteli ya Emirates Palace huko Abu Dhabi.Picha: AP

Rais George W Bush wa Marekani leo anaelekea nchini Saudi Arabia kujaribu kutafuta uungwaji mkono katika mazungumzo ya kutafuta amani kati ya Israel na Palestina na kuendeleza shinikizo la Marekani dhidi ya Iran. Wakati huo huo rais wa Ufaransa Nicolas Sarkozy naye anaanza ziara yake rasmi katika nchi tatu za ghuba kwa kuitembelea Saudi Arabia.

Rais George W Bush anataka kuishawishi Saudi Arabia ishiriki kikamilifu katika mchakato wa kutafuta amani kati ya Israel na Palestina na kujaribu kuendeleza shinikizo dhidi ya jamhuri ya kiislamu ya Iran. Rais Bush atakaa kwa siku mbili nchini Saudi Arabia huku akiwa tayari amezitembelea Kuwait, Bahrain na jumuiya ya falme za kiarabu.

Ujumbe wa rais Bush kwa washirika wake wa eneo la ghuba umekuwa kuwashawishi waziunge mkono juhudi za amani na waitenge Iran ili kudhibiti ushawishi wake unaoendelea kuongezeka katika eneo hilo, ambalo ni muhimu kwa usafirishaji wa mafuta duniani kote.

Rais Bush ameonya juu ya kile alichokiita kitisho kwa dunia kinachosababishwa na Iran, akisisitiza kwamba ipo haja ya kukabiliana na Iran kabla mambo kufikia mahala pabaya. Aidha rais Bush amesema Marekani inaziongezea nguvu mpya juhudi zake za kuwalinda washirika wake katika eneo la ghuba. Ameileza Iran kama nchi inayoongoza katika kudhamini ugaidi duniani.

´Iran leo ni nchi inayoongoza katika kudhamini ugaidi. Inatuma mamia ya mamilioni ya dola kwa magaidi kote duniani huku Wairan wakikabiliwa na hali ngumu ya maisha na matatizo ya kiuchumi nchini mwao. Inavuruga juhudi amani nchini Lebanon kwa kulipa silaha na kulidhamini kundi la kigaidi la Hezbollah.´

Waziri wa mashauri ya kigeni wa Iran, Manouchehr Mottaki amesema juhudi za rais Bush kuvuruga uhusiano wa Iran na nchi jirani za kiarabu hazitafua dafu na kuipuuza ziara ya rais Bush katika eneo la Mashariki ya Kati akiitaja kuwa kazi bure.

Hii leo rais Bush amejionea kwa macho eneo lililo mashuhuri kwa biashara na sekta ya benki duniani la Dubai, ambalo majumba yake marefu ya vioo na ujenzi wa majumba ya kisasa umeigeuza Dubai kuwa mji mkuu wa eneo la Mashariki ya Kati. Kabla kwenda Dubai rais Bush ameanza shughuli zake za leo kwa kukutana na viongozi wa kibiashara wa Abu Dhabi. Ameisifu jumuiya ya nchi za kiarabu kwa juhudi zake za kutafuta nishati mbadala badala ya kutegemea mafuta pekee.

Akiwa Abu Dhabi rais Bush alizungumzia swala la demokrasia na kulilaumu kundi la al Qaeda kwa kuvuruga demokrasia katika eneo hilo.

´Sababu nyingine kubwa ya ukosefu wa uthabiti ni itikadi kali inayoendelezwa na kundi la al Qaeda na washirika wake. Tunajua kwamba demokrasia ndiyo aina pekee ya serikali inayowapa watu heshima na usawa ambao ni haki yao.´

Kutoka Saudi Arabia rais Bush ataelekea nchini Misri kabla kurejea mjini Washington.

Wakati huo huo, rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy, yumo mjini Riyadh Saudi Arabia katika ziara yake ya kwanza tangu alipoingia madarakani mnamo mwezi Mei mwaka jana. Rais Sarkozy anafanya ziara yake ya siku tatu katika nchi za eneo la ghuba wakati rais Bush wa Marekani akifanya ziara yake ya siku nane katika eneo la Mashariki ya Kati.

Rais Sarkoz amewaambia waandishi wa habari mjini Riyadh kwamba Saudi Arabia ni kiungo muhimu cha amani Mashariki ya Kati, baada ya kusaini mikataba ya ushirikiano na serikali ya Saudi Arabia. Baadaye leo anatarajiwa kukutana na wafanyabiashara wa kifaransa na wa Saudi mjini Riyadh kabla kuondoka kwenda Qatar.

Hapo kesho rais Sarkozy atasafiri kwenda jumuiya ya nchi za kiarabu ambako anatarajiwa kusaini mikataba ya ushirikiano katika maswala ya nishati ya nyuklia.