1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais dhidi ya waziri mkuu

Maja Dreyer10 Aprili 2007

Mvutano ndani ya serikali ya Ukraine unaendelea na bado suluhisho liko mbali. Rais Yushchenko alilivunja bunge na akatangaza uchaguzi upya utafanyika. Wingi wa bunge na wa baraza la mawaziri chini ya waziri mkuu Yanukowitsh wanaipinga hatua hiyo wakiungwa mkono na waandamanaji 30.000 waliofika mji mkuu Kiev hii leo.

https://p.dw.com/p/CHGc
Waandamanaji mjini Kiev
Waandamanaji mjini KievPicha: AP

Leo asubuhi, mabasi na treni zimefika katika mji mkuu wa Ukraine, Kiev, zikiwasafirisha wafuasi wa vyama tawala wakitoka hasa eneo la Mashariki mwa Ukraine. Huko watu wengi wanaoongea Kirusi wanampinga rais Yushchenko. Lakini hali mjini Kiev iliendelea kuwa shwari na biashara za kila siku ziliendelea kama kawaida. Chama cha rais Yushchenko kilitangaza kitafanya maandamano makubwa kesho Jumatano.

Licha ya maandamano dhidi yake yaliyoendelea hata kwenye sikukuu za Pasaka, rais Yushchenko hakubadilisha amri yake ya kufanywa uchaguzi mpya mwezi wa Mei.

Jana usiku, bunge la Ukraine, ambalo limevunjwa na rais, limepitisha azimio la kukubali uchaguzi wa mapema ikiwa rais pia atachaguliwa upya. Wakati huo huo, bunge lilidai kufanwe kura ya maoni juu ya kujiunga na jumuiya ya magharibi ya ulinzi, NATO.

Ikiwa uchaguzi wa rais ungefanyika, rais Yushchenko anasemekana kuwa na fursa ndogo tu ya kuchaguliwa tena. Kwa hivyo hakuna matumaini kuwa Yushchenko atakubali azimio hilo. Juu ya hayo, Yushchenko ameshaarifu kuwa chochote kilichopitishwa na bunge hili hakina maana yoyote, kwa vile alilivunja bunge tangu tarehe 2 Aprili. Waziri mkuu Victor Yanukowitsh, sehemu kubwa ya mawaziri na ya wabunge wanapinga hatua hii wakisema ni kinyume na katiba.

Mahakama ya katiba ya Ukraine yanatarajiwa kuanza kesho kusikiliza kesi juu ya hatua ya rais ya kulivunja bunge. Katika mkutano na waandishi wa habari leo hii, mahakimu watano wa mahakama haya wamesema wanashurutishwa na wabunge na kuomba ulinzi wa polisi ili usalama wao uhakikishwe.

Mahakama ya katiba ya Ukraine ina mahakimu 18, sita kati wao wakiteuliwa na bunge, sita wengine na rais na sita wengine wanateuliwa na halmashauri inayotakiwa kuwa bila ya upendeleo. Ili kutoa hukumu kura kumi zinahitajika. Mahakimu hawa watano wote wanaaminika wanamuunga mkono rais Yushchenko. Ikiwa wanaamua kususia kesi hiyo, hukumu yoyote itakayotolewa haitakuwa na uzito. Rais Yushchenko pia amelaumiwa kuwashinikiza mahakimu.

Yushchenko na mpinzani wake waziri mkuu Yanukowitsh walikutana leo kwa mazungumzo, lakini kwa mara nyingine tena mkutano kati wao ulimalizika bila ya matokeo.