1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Donald Trump alilaumu Shirika la Afya Duniani WHO

Zainab Aziz
8 Aprili 2020

Rais Donald Trump amelishukia shirika la afya duniani WHO na kulilaumu kwa kuegemea upande wa China.Trump amesema asasi hiyo ya kimataifa ilishirikiana na China kuficha ukweli. 

https://p.dw.com/p/3ac7v
USA Coronavirus US-Präsident Donald Trump
Picha: picture-alliance/CNP/AdMedia/J. LoScalzo

Rais wa Marekani Trump ametishia kulikatia fedha shirika la afya Duniani WHO kwa sababu amesema shirika hilo halikutilia maanani kwa namna ilivyopasa hatari ya maambukizi ya virusi vya corona. Trump amelilaumu shirika hilo kwa kuegemea zaidi upande wa China. Rais huyo wa Marekani amedai kwamba asasi hiyo ya kimataifa ilishirikiana na China katika miezi kadhaa iliyopita kupuuza hatari ya maambukizi ya virusi vya corona.

Akitoa taarifa juu ya hali ya maambukizi hayo nchini Marekani, Trump alipuuza umuhimu wa taarifa ya mshauri mwandamizi iliyotolewa mapema mwaka huu kutahadharisha juu ya uwezekano wa kulipuka kwa maambukizi hayo. Rais huyo amedai kwamba hakuiona taarifa hiyo.

Badala yake Rais huyo wa Marekani amelishukia shirika la afya duniani WHO na kulitishia kulikatia fedha.Trump amesema asasi hiyo inaegemea sana upande wa China kuhusu mkakati wake wa kupambana na maambukizi ya virusi vya corona. Amedai kwamba Shirika la WHO lilishirikiana na China katika juhudi za nchi hiyo za kupunguza hatari ya mlipuko wa maambukizi hayo.

Rais Trump amesema Shirika hilo limeisifu China ingawa pana sababu ya kuwa na mashaka juu ya idadi rasmi  iliyotolewa na serikali ya China juu ya vifo vilivyotokana na mambukizi ya virusi vya corona.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus
Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom GhebreyesusPicha: Getty Images/AFP

Trump amesema WHO ilipaswa kujua juu ya hayo.Tangu aingie madarakani Rais Trump amekuwa anayatilia mashaka mashirika ya kimataifa na mara kwa mara amekuwa analibeza shirika  hilo la afya. Katika bajeti ya mwezi Februari utawala wa Trump ulipendekeza kupunguza mchango wa fedha wa Marekani kwa shirika la WHO kutoka dola milioni 122.6 hadi dola milioni 59.9

Shirika hilo la kimataifa lililitangaza mlipuko wa maambukizi ya virusi vya corona kuwa hatari kwa afya ya binadamu wote, tarehe 30 mwezi Januari, takriban mwezi  mmoja kabla ya rais wa Marekani kusema kwenye "twitter” kwamba maambukizi ya virusi vya corona yalikuwa yamedhibitiwa nchini Marekani.

Mpaka sasa watu zaidi ya alfu 12 wameshakufa kutokana na maambukizi  ya virusi vya  corona nchini Marekani na wataalamu wa masuala ya afya wamesema idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka wiki hii nchini Marekani.

Rais Trump ameendelea kutetea njia alizotumia katika juhudi za kupambana na mambukizi ya virusi vya corona na ameendelea kupuuzia taarifa ya tahadhari iliyotolewa na mshauri mwandamizi Peter Navarro juu ya uwezekano wa kulipuka kwa maambukizi ya corona. Mshauri huyo alitanabahisha kuwa mlipuko wa maambukizi hayo utaigharimu Marekani mambilioni ya fedha na vifo vya Wamarekani wengi. Hata hivyo Trump amesema ingelikuwa mapema mno kuchukua hatua na kwamba hakutaka kuwatia watu wasi wasi.

Chanzo:/ AP